BEKI wa Kimataifa wa Kenya, Joash Onyango amerejea kikosini baada ya kutokuwa sehemu ya kikosi hicho kwa takribani wiki 2.
Onyango amerudi kujiunga na kikosi cha Mnyama kilichotoka Malawi kucheza mechi yake ya kwanza ya Klabu bingwa, na hivyo atasafiri na timu kwenda Sumbawanga kwaajili ya mchezo wa raundi ya nne wa Ligi kuu ya NBC.
Kwa taarifa tulizonazo, sababu ya Beki huyo kufanya mgomo baridi ni kutokana na kuwekwa benchi na aliyekuwa kocha mkuu wa Simba SC Zoran Maki, kitu ambacho Onyango hakukipenda na kilikuwa kinamnyima furaha klabuni hapo, na ndipo alipochukua uamuzi wa kuandika barua TFF kuomba haki itendeke ili yeye aondoke.
Hali hiyo ndiyo iliyomsukuma kugomea mazoezi na timu au kuwa sehemu ya timu na kutaka kuondoka, ila urejeo wake kikosini inamaanisha mambo ni mazuri.
Lakini Kamati ya Sheria, Wanachama na Hadhi za Wachezaji ya TFF, iliamuru kuwa Mchezaji huyo arejee Kikosini na kuendelea na maisha yake ya kiuchezaji akiwa na Simba SC.
Msemaji wa Wekundu Ahmed Ally alipoulizwa na chombo cha habari cha Wasafi, kuhusu muenendo wa mchezaji huyo alisema kuwa “Ni kweli hali ya kukaa benchi sio nzuri kama mchezaji lazima asiwe na furaha nayo”.

Simba SC watacheza mchezo wao wa raundi ya nne wa Ligi Kuu ugenini dhidi ya wajelajela Tanzania Prisons, baada ya hapo watarejea Dar ES Salaam kujiandaa na mechi ya mkondo wa pili ya CAFCL dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi itakayochezwa Tarehe 17 Septemba 2022.