Wakala wa nyota huyo anayekipiga klabu ya Madrid anasema mipango ya klabu hiyo inaenda kama wanavyohitaji kuifanya wao iende na wamegoma kabisa kumuuza nyota huyo na kwamba bado wanahitaji huduma yake msimu ujao na hawawezi kumuuza kwa namna yoyote ile.
Msimu wa 2018/19 haukuwa na mafanikio kabisa kwa nyota huyo na kikosi cha Madrid kwa ujumla. Nyota huyo hakupata nafasi zaidi kuonesha uwezo wake uwanjani kwenye mechi nyingi jambo ambalo lilionekana kama lingemfanya ashawishike kuondoka lakini Zidane amekanusha taarifa hizo na bado anamhitaji.
Kwa mujibu wa wakala wa mchezaji huyo, Horacio Gaggioli, anasema miamba hao wa soka nchini Hispania wamegoma kabisa kufanya biashara ya mchezaji huyo hata kwa uhamisho wa €180m kutoka kwa klabu zilizokuwa zinamhitaji nyota huyo. Jambo hilo linaonesha uhitaji walionao juu ya nyota huyo msimu ujao.
Hadi sasa ameanza mechi 20 pekee kati ya 42 za ligi na klabu bingwa jambo ambalo haijawahi kutokea kwa nyota huyo kwenye maisha yake ya soka ndani ya klabu hiyo. Jambo hilo linapelekea ushindani uwe mkubwa zaidi ndani ya kikosi cha Madrid kutokana na uwepo wa wakongwe ndani ya kikosi.
Klabu ambazo zilionekana kumtolea macho nyota huyo ni pamoja na Juventus na Liverpool lakini ripoti zilizotoka ni kwamba si klabu wala nyota mwenyewe wa klabu hiyo anawiwa kuondoka klabuni hapo, pande zote mbili zipo tayari kuendelea kufanya kazi pamoja ndani ya ardhi ya Madrid.
Inakumbukwa kwamba Madrid walitimua makocha wawili nyakati tofauti lakini wakaona ni wakati muafaka wa kumteua kwa awamu nyingine Zidane ambaye alishinda mataji makubwa mfululizo akiwa na klabu hiyo. Kwa sasa wamemtengea dau nono kuhakikisha anafanya usajili mkubwa ili kunusuru heshima ya kikosi chao hicho kutokana na mwenendo mbovu waliokuwanao.
Ili kutambua nafasi yake Asensio amepewa nafasi ya kucheza mechi zake tano kati ya sita akiwa na kocha huyo. Jambo jingine ambalo ni kubwa zaidi ni kwamba pamoja na kukosa nafasi kwa makocha waliopita tayari kikosini hapo bado amekuwa na thamani chini ya kocha wake wa kikosi cha timu ya taifa Luis Enrique na amempa nafasi ya kucheza hata kwenye hatua ya kutafuta nafasi ya kufuzu iliyofanyika Machi mwaka huu.
Kwa hakika ni aina ya wachezaji ambao sio rahisi kwa klabu kama Madrid kuwauza haraka kwa sababu wanajua majukumu yao na wanatambua nafasi yao wakiwa uwanjani. Anachoamini Zidane ni kwamba nyota huyo kwa sasa anafikiri zaidi juu ya nini cha kufanya msimu ujao.


Povel
Duh noma sana