NI piga nikupige ndani ya ligi kuu ya Uingereza msimu huu na kuonekana kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na tofauti ya alama iliyokuwepo kati ya klabu moja na nyingine kati ya zile zilizokuwa zikipigania nafasi nne za juu kwa hakika ilinogesha ligi hiyo kwa aina fulani ya matokeo ambayo yalivutia zaidi ligi hiyo.
City ameweza kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululuzo katika misimu miwili wakiwa chini ya Pep ambaye amekuwa na uwezo mkubwa wa kurudisha heshima ya kikosi hicho kwa miaka ya hivi karibuni baada tu ya kupokea kikosi hicho na kukijenga kwa kufanya usajili wa aina yake uliowasaidia sana kufika hapo.
Wameweza kulinda taji hilo baada ya kulishinda msimu uliopita baada ya ushindi wa 4-1 walioupata mbele ya Brighton na kufanikiwa kuandika historia mbele ya ligi hiyo ya Uingereza kwa kuweza kunyanyua taji hilo mfululizo baada ya historia hiyo kufunikwa kwa miaka mingi.
Aina hiyo ya ushindi iliwahi kutokea msimu wa 2008/9 pale iliyokuwa Manchester ya Sir. Alex ilipokuwa kwenye uwezo wa juu sana na kufanikiwa kuiteka dunia kisoka hapo ndipo jambo hilo la kihistoria liliweza kutokea. Baadaye ilikuwa ni kwa msimu mmoja klabu inachukua na kubadilishana na nyingine.
City, kwa sasa, wana mataji manne ndani ya miaka nane na wana kila sababu ya kuzidi kutawala soka la Uingereza chini ya Pep. Hiyo ni kutokana na aina ya kikosi alichonacho ambacho tayari kimejenga kuelewana ndani ya uwanja. Pia, takwimu zao za alama kwa msimu uliopita (100) na msimu huu (98) ni kipimo tosha kabisa kwa timu hiyo kuwa bora sana.
Washindi hao wa EFL kwa sasa watarudisha nguvu zao zote kwenye kombe la FA ambalo watakuwa uwanjani kucheza fainali na Watford pale Wembley na hii imetokana na kampeni nzuri waliyoifanya ndani ya msimu huu. Wana kila kitu cha wao kunyanyua kombe hilo na kuandika historia nyingine tena.
Liverpool wanaendelea na maumivu yao ya miaka 29 bila kunyanyua kombe hilo la 19 la ligi kwao na katika historia wanabaki tu kusogea hadi nafasi ya kulinyakua lakini siku zinavyozidi kwenda wanakosa kabisa nafasi yao hiyo na kuambulia kutazama wengine wakiendelea kukusanya vikombe huku yeye akiwa kama mtazamaji pekee.
Kutokana na ushindi huo hatuna budi kuwapa hongera Manchester City kwa kunyanyua ndoo hiyo kwa awamu nyingine. Lakini pia bila kuwasahau Cardiff City, Fulham na Huddersfield kwa kuporomoka daraja na kurudi kucheza Championship msimu ujao. Katika mchezo lazima mmoja ashindwe kumuachia mwingine.

