Klabu ya Manchester City imefanikiwa kukaa kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingereza baada ya kufanikiwa kushinda mchezo wao dhidi ya klabu ya Fulham mchezo uliopigwa katika dimba la Craven Cottage.
Manchester City wameshinda mchezo wao dhidi ya Fulham kwa mabao mawili kwa moja magoli ya Earling Haaland pamoja na Julian Alvarez huku goli la kufutia machozi la Fulham likifungwa na Vinicius, Kupitia ushindi huo City wanakwea kileleni na kuishusha Arsenal waliokaa kwenye usukani kwa muda mrefu.
Vijana wa Pep Guardiola wamepanda kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha alama 76 alama moja mbele ya klabu ya Arsenal,Huku klabu hiyo ikiwa na mchezo mmoja mkononi lakini wameweza kwenda kileleni kwenye msimamo wa ligi kuu ya Uingereza mbele ya vijana wa Mikel Arteta.
Manchester City wapo kwenye fomu nzuri hivi karibuni baada ya kufanikiwa kushinda michezo nane mfululizo ya ligi kuu ya Uingereza, Baada ya kushinda michezo hiyo mfululizo iliweza kuwarudisha vijana hao wa Pep Guardiola kwenye mbio za ubingwa na kukaa kileleni kwenye msimamo.
Klabu ya Manchester City mpaka sasa wapo kwenye nafasi nzuri ya kushinda mataji matatu ndani ya msimu mmoja na kuvunja rekodi ya majirani zao klabu ya Manchester United ya mwaka 1999, City mpaka sasa wanaongoza ligi, wapo fainali ya kombe la Fa na wapo nusu fainali ya ligi ya mabingwa ulaya.

