Klabu ya Manchester United leo itashuka dimbani katika dimba la Old Trafford kuwakaribisha klabu ya Real Betis kutoka nchini Hispania katika mchezo wa kombe la Uefa Europa League.
Maswali ni mengi kua Manchester United inaweza kurudi kwenye njia yake ya ushindi dhidi ya Real Betis leo baada ya kupokea kichapo kizito kwa klabu ya Liverpool wikiendi iliyomalizika, Man United watakua na faida ya kuwepo katika dimba lao la nyumbani leo dhidi ya Betis.
Manchester United wamekua na rekodi nzuri katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu kwani hawajapoteza mchezo katika michuano yote kwenye michezo 20 iliyopita, Hivo inaweza kua faida kwa upande wao kutokana na rekodi yao nzuri kwenye uwanja wa nyumbani.
Mashetani Wekundu baada ya kupoteza dhidi ya Liverpool wikiendi iliyomalizika kwa kipigo cha aibu inadhaniwa kua inaweza kuwatoa kwenye njia, Kwani klabu hiyo ilikua ina mwenendo mzuri kabla ya kupoteza dhidi ya Liverpool na mchezo wa leo dhidi ya Real Betis ndio utatoa majibu sahihi.
Manchester United leo watashuka dimbani wakiwa na taarifa nzuri kwani mshambuliaji wao raia wa kimataifa wa Ufaransa Anthony Martial amerejea kwenye mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake baada ya kukosekana katika michezo kadhaa iliyopita kutokana na majeraha yaliyokua yanamuandama.

