LEONEL Ateba mshambuliaji wa Simba amesema kuwa furaha yake ni kuona timu hiyo inapata ushindi na watapambana kufikia malengo ikiwa ni pamoja na kutwaa ubingwa.
Ipo wazi kwamba Ateba kibindoni katupia mabao matano ambapo katika hayo matatu ni kwa mapigo ya penalti msimu wa 2024/25 na ametoa pasi moja ya bao akihusika kwenye mabao sita kati ya 24 yaliyofungwa na timu hiyo.
Kwenye mchezo dhidi ya Ken Gold, Ateba alitupia mabao mawili, dakika ya 34 kwa mkwaju wa penalty iliyosababishwa na Awesu Awesu na dakika ya 44 kwa pigo la kichwa.
Ateba amesema wanatambua ushindani ni mkubwa ndani ya ligi hivyo wanapambana kupata matokeo mazuri kila wakati kwa ushirikiano na wachezaji wengine.
“Tunatambua ushindani ni mkubwa na kila timu inahitaji kuona kwamba inapata matokeo mbele yetu kama ambavyo nasi tunahitaji ushindi mbele yao, kila wakati tunafanya kazi kubwa kupata ushindi tunashukuru mashabiki wapo pamoja nasi hivyo tutaendelea kupambana.”