Safari ya kuelekea Kombe la Dunia 2026 imechukua sura mpya baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) kuiondoa Nigeria kwenye hatua za mchujo kwa ushindi wa mikwaju ya penalti. Katika mchezo uliopigwa Rabat, Morocco, Wacongo walionyesha ubora wa hali ya juu na kushinda 4–3 kwenye mikwaju ya penalti baada ya sare ya 1–1 ndani ya dakika 120.
Nigeria, waliokuwa wanaonekana bora kwenye makaratasi kutokana na nafasi yao ya juu kwenye viwango vya FIFA, waliingia kwa kasi na kupata bao la mapema kupitia shuti la Frank Onyeka lililomgonga Axel Tuanzebe na kumuacha kipa Lionel M’Pasi. Hata hivyo, DR Congo hawakuruhusu bao hilo la mapema kuwaangusha.
Walipanga upya mchezo wao, wakatafuta nafasi na hatimaye Mechak Elia akasawazisha dakika ya 32 baada ya uzembe wa nahodha wa Nigeria, Wilfred Ndidi, kwenye eneo la hatari. Kuanzia hapo, upepo wa mchezo uligeukia upande wa Wacongo.
Kadri dakika zilivyozidi kusonga, DR Congo walionekana kujiamini zaidi, hasa baada ya Nigeria kumpoteza mshambuliaji wao hatari Victor Osimhen kutokana na majeraha mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Kasi ya Wacongo iliwalazimu Nigeria kucheza kwa tahadhari, lakini bado iliwacharaza jasho kwenye dakika ya 83 baada ya makosa ya kipa Stanley Nwabali yaliyokaribia kuwamaliza.
Katika dakika za nyongeza, DR Congo walidhani wamepata bao la pili, lakini mwamuzi wa Morocco akalikataa kwa madai ya faulo kabla ya mfungaji Noah Sadiki kumalizia mpira wavuni.
![]()
Bila kusahau meridianbet ndio wakali wa ODDS KUBWA, Machaguo zaidi ya 1000 na kila kitu ukitakacho. Bashiri kijanja hapa
Kipindi cha penalti kiligeuka kuwa tamthilia ya ushujaa. Kocha wa DR Congo alifanya uamuzi wa kifundi kumtoa M’Pasi dakika ya mwisho ya muda wa ziada na kumuingiza Timothy Fayulu, uamuzi uliolipa baada ya kipa huyo mpya kuokoa penalti mbili muhimu.
Kwa ushindi huo, DR Congo sasa watashiriki mashindano maalum ya mchujo wa mabara sita yatakayofanyika Guadalajara na Monterrey, Mexico mnamo Machi 2026. Watakuwa miongoni mwa mataifa sita yatakayowania tiketi mbili za mwisho kuelekea Kombe la Dunia.



