Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amemkosoa kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler, baada ya kudai kuwa Arsenal “wanajiwekea sheria zao wenyewe” kufuatia ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Brighton & Hove Albion katika uwanja wa Amex Stadium Jumatano.

Bao la Bukayo Saka lililobadilisha mwelekeo baada ya kuguswa na mchezaji wa Brighton mapema katika kipindi cha kwanza, lilitosha kuipa Arsenal FC ushindi wa tatu mfululizo katika Premier League na kuongeza nafasi yao ya kutwaa ubingwa.

Ushindi huo umeifanya Arsenal kuongoza msimamo kwa tofauti ya pointi saba dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City waliopo nafasi ya pili, baada ya City kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Nottingham Forest.
Licha ya matokeo hayo mazuri, Hurzeler aliikosoa Arsenal kwa kuchelewesha mchezo kwa makusudi na kudai kuwa walikuwa wakijifanya kuumia ili kupoteza muda. Alimtaja kipa wa Arsenal, David Raya, kuwa alianguka mara kadhaa na kuhitaji matibabu jambo lililoibua tuhuma za kupoteza muda ili Arteta apate nafasi ya kutoa maelekezo kwa wachezaji wake.

Akijibu tuhuma hizo, Arteta alisema hajali ukosoaji huo na kusisitiza kuwa anajivunia wachezaji wake kwa namna wanavyopambana uwanjani. Aliongeza kuwa ni kawaida kwa wapinzani kujaribu kuisumbua timu inayokuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Kwa sasa Arsenal wanaendelea kuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa taji lao la kwanza la ligi tangu mwaka 2004, huku pia wakiendelea kushiriki mashindano mengine ikiwemo UEFA Champions League na FA Cup.


