Real Madrid wameanza vyema safari yao ya matumaini chini ya meneja Zinedine Zidane anayehudumu kwa kipindi cha pili baada ya aliyekuwa meneja wa klabu hiyo Santiago Solari kutimuliwa. Real wameanza kwa kushinda gemu yao ya kwanza chini ya Zidane kwa mara nyingine.
Mfaransa huyu alisepa akiwa amewaongoza Real Madrid kunyakua ubingwa wa Ulaya mara tatu mfululizo lakini Real wameshindwa kuendeleza moto huo chini ya Solari wakijikuta wametupwa nje kabisa ya michuano hiyo.
Magoli ya Isco na Gareth Bale yalitosha kabisa kumpa furaha zidane anayehudumu kwa mara ya pili klabuni hapo.
Matumaini yatazaa matunda?
Zidane ameingia akiwa na mipango mikubwa ya kurejesha heshima ya klabu hiyo, kuna taarifa kuwa klabu pia ipo tayari kumpa bunda la pesa atakazozihitaji kwa ajili ya usajili kwa ajili ya kuweka sawa kikosi chake.
Kwa sasa macho ya Zidane yanaangalia msimu ujao zaidi kwa ajili ya kupambana kwenye ligi ya mabingwa ulaya. Kwa upande wa La Liga, Real Madrid wapo nafasi ya 3 wakiwa nyuma ya Atletico Madrid kwa pointi 2. Kwa gemu ambazo zimebakia wanaweza kumpindua Atletico Madrid kama watashinda gemu nyingi zilizobakia na kumuombea njaa Atletico, lakini kuupata ubingwa ni kazi zaidi kwa moto walio nao Barcelona na gemu ambazo zimebakia.

