Baada ya michezo yote kumalizika huku baadhi ya klabu zikivunja historia kubwa za ushiriki ndani ya michuano hiyo ya klabu bingwa Afrika sasa shirikisho la mpira wa miguu Afrika limepata timu zake zinazotakiwa kuingia hatua ya robo fainali ili kupata wawakilishi watakaokutana nusu fainali baada ya hatua hiyo muhimu.
Michuano hiyo mara nyingi huwa ni hatua pekee inayofanya soka la Afrika lipate heshima pia husaidia kutambulisha wachezaji na kuzifanya klabu mbalimbali kurusha macho yao kusajili wachezaji hao wacheze soka la kulipwa nje ya nchi zao. Jambo hili huwa ni ndoto ya kila mwanasoka kwani humfanya ajifunze mengi kutoka kwa wachezaji wa mataifa mbalimbali na kujifunza miiko mingine ya kisoka zaidi ya vile ilivyozoeleka.

Kuna wachezaji wengi waliopata nafasi ya kucheza kwenye klabu nyingi kubwa za nje ya nchi ikiwa ni zao la michuano hiyo mikubwa. Hivyo hatuna budi kuithamini michuano kama hii kwa sababu ni ramani ya wanamichezo wengi, hususan inapofikia hatua hiyo hurushiwa jicho la pekee kwa sababu ni wakati ambao klabu zenye wachezaji wenye uwezo mkubwa hukutana katika hatua hiyo.
Kila mtu anajua wa kukutana naye
Makundi ya hatua hiyo ya robo fainali yamepangwa kwa sasa na kila klabu imeshajua nani wa kukutana naye kuelekea katika hatua hiyo. Upangaji huo umezingatia vigezo vyote na kila klabu itacheza mechi mbili nyumbani na ugenini. Washindi watakaopatikana hapo wataelekea hatua ya nusu fainali. Makundi hayo ni:
CS Constantine (Algeria) watakutana na Esperance (Tunisia), mechi hii inategemewa kuwa yenye ushindani mkubwa kutokana na uzoefu wa klabu hizi mbili na uwezo wa kila klabu kupata matokeo. Jambo hilo litafanya mechi hiyo iwe ni yenye kuvutia na yenye ufundi wa kila aina. Tutegemee soka safi kupitia wao.
Mamelodi Sundowns (South Africa) dhidi ya Al Ahly (Egypt), ni miongoni mwa pambano linalotegemewa kuvuta hisia za mashabiki wengi kutokana na historia kubwa za klabu hizi mbili. Wamisri wana uzoefu mkubwa ndani ya michuano hiyo kitu ambacho kinawapa nafasi kubwa ya kusonga mbele zaidi ndani ya michuano hiyo japo michuano ya mwaka huu ni tofauti kidogo.
Horoya (Guinea) watapambana na Wydad Athletic Club (Morocco), kwa kipindi cha hivi karibuni miamba wa soka wa Guinea hawajawa na historia inayoeleweka sana. Japo kwa kipindi cha nyuma walisumbua sana na huenda wakawa wamekuja na ujio mpya kuweza kuandika historia upya pamoja na kwamba Wamorocco hao sio wa kubeza.
Simba (Tanzania) dhidi ya TP Mazembe (DR Congo), klabu hiyo ya Tanzania imerudi kwenye ramani hivi karibuni ikiwa ni baada ya miaka mingi sana kufanya vibaya ndani ya michuano hiyo. Ujio huo umewashtua wengi kutokana na mapinduzi waliyoyaonesha hadi kufikia hapo. Wanakutana na wababe wa Congo ambako mchezaji wao wa zamani alipata nafasi ya kuwatumikia hivyo tutegemee upinzani mkubwa sana.


Furahav
Ni kweli kila mchezaji huwa anapenda kucheza timu ya Taifa.
Povel
Habar njema