Waingereza wanalipenda sana soka kuliko hata linavyowapenda, kuna wakati mpira unawakubali na kuwapa wanachotaka ila kuna wakati sasa loooooh salaleee. Amini usiamini sijui huwa mpira una nini kwa Waingereza, kuna kipindi walikuwa wanakutana timu 3 kutoka Uingereza tena nusu fainali kwenye klabu bingwa ulaya na bado kombe halirudi kwao, hakuna la ajabu hapo kwani msimu wa 2009 Barcelona alichukua kombe mbele ya Man United pale Roma.
Kuna kipindi mambo huwa magumu kabisa kwani hushindwa kupenya hata hatua ya robo fainali, ndiyo msimu wa 2012/13 ulikuwa mgumu haswa kwa Waingereza ulaya. Sasa ngoja uhadithiwe misimu ya raha haahaahaa Waingereza watakutana wenyewe fainali, mfano 2008 Chelsea na Man United Waingereza walijua tu kuwa kombe linarudi kwao vyovyote iwavyo.
Tusiende mbali sana msimu uliopita ulikuwa wa raha zaidi kwa Waingereza maana Liverpool na Tottenham walicheza fainali Ulaya huku Arsenal na Chelsea wakicheza fainali Europa Cup, Mungu awape nini tena Waingereza, furaha iliyoje tuseme hapa kichaa kilitulia.
Ila msimu huu naona kichaa kimepanda mapema yaani asubuhi tu wazimu ulishawehuka Wazungu husema, “Sometime yes, sometime no!” ndiyo hii sasa maana dalili zote zinaonekana kuwa huu ni mwaka wa no hasa hasa klabu bingwa.
Alianza mapema Arsenal katika hatua ya 32 bora kule Europa, ajabu kuwa alianza kupata ushindi ugenini na Olympiacos Pirateas wa goli moja bila akaja kukubali kichapo nyumbani kwa 2-1 shughuli ikaishia hapo hapo wasijue la kufanya. Ikabidi wawaachie kazi Man United na Wolverhampton Wanderers waendeleze gurudumu la kuhakisha Europa linarudi tena Uingereza.
Shughuli ikabaki kwa wakubwa waliopo klabu bingwa Ulaya, huku mashaka yalikuwa zaidi kwa Man City na Chelsea kwani walipangiwa vigogo haswaaa ila Tottenham na Liverpool hofu wala haikuwa kubwa. Ila kwa kuwa historia zimewekwa ili zivunjwe, Man City wakatushangaza kabisa tena mshangao ule wa kuacha watu midomo wazi, ndiyo tulishangaa maana kumfunga Real Madrid katika dimba la Bernabéu siyo kazi rahisi ila ukweli City waliibuka na ushindi wa bao 2-1 ugenini.
Upande wa Chelsea mambo yalienda kama tulivyotarajia, Chelsea alikufa goli 3 kavu au bila majibu pale Darajani, tuseme kumkabili Bayern Munich kwa sasa ni kazi ngumu siyo ya kitoto, kumlaumu Lampard ni kumuonea tu, muache apevuke kwanza.
Liverpool na Tottenham ndiyo wameleta songombingo au hali ya sintofahamu, kiufupi wao wameshaondolewa kwenye mashindano, afadhali Chelsea na Man City wao wana mechi za marudiano. Tottenham yeye mapema tu alikubali kichapo cha goli moja kwa buyu pale London, wengi tukaamini labda Mourinho ataleta miujiza kule Ujerumani. Ila mambo yakawa tofauti kabisa maana kule Ujerumani akakumbana na kichapo cha kufa mtu cha mabao 3-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 4-0, Muingereza wa kwanza huyo akafurushwa nje ya mashindano.
Kesho yake Liverpool akaingia mzigoni kumkabili Atletico Madrid, Liverpool akiwa na kumbukumbu ya kichapo cha bao moja kwa nunge alichokipata ndani ya dimba la Wanda Metropolitano pale Madrid katika mchezo wao wa kwanza. Hii ilikuwa ni nafasi sasa ya kulipiza kisasi au kuuaminisha umma kuwa hakumfunga Barcelona zile goli 4 kwa kubahatisha. Ndani ya Anfield Liverpool alipata bao moja tu ndani ya dakika tisini hivyo matokeo kuwa 1-1, muamuzi akaamuru dakika 30 ziongezwe.
Kipute kikaanza upya, mapema tu Firmino akaweka mpira wavuni na kufanya ubao kusomeka 2-1 dakika ya 94 hiyo. Lah, haula wala kuwata tuseme kuwa walichokoza nyuki kwani Atletico kupitia mchezaji wao wa akiba Llorente alipiga bao mbili za haraka na kupika bao moja hivyo kufanya matokeo kuwa 2-3 na mpira ukaisha hivyo hivyo matokeo ya jumla yalisomeka 4-2, Liverpool out.
Tuseme tu shughuli imebaki kwa Guardiola na Man City yake, huku kwa Chelsea mmmmh sidhani maana siyo dua tu pia miujiza inahitajika ili kupata matokeo pale jijini Munich. Chelsea ashinde goli tatu bila ili waende hatua ya penati, hivi Lewandoski, Muller na kale katoto ka Gnabry kanachopenda kuzifunga timu za London watakuwa wamesimama au, hapa dua tu na miujiza, si vinginevyo. Man City ndiyo tunampa dhamana angalau tupate Muingereza mmoja katika hatua ya robo fainali.
Guardiola namuaminia hasa kwa kuwa yupo nyumbani ila Zidane ananipa ukakasi kidogo kuamini kuwa ataondolewa kwenye hatua hii mmmh napata shida kidogo kuamini japo mpira unadunda. Naamini shughuli itakuwepo wiki ijayo katika dimba la Etihad pale jijini Manchester ama kwa hakika nyasi zitawaka moto.
Mungu Hakunyimi vyote, pengine Waingereza wanaweza kusema hivyo, kwani Europa ligi kidogo linatoa matumaini ya kulibakisha kombe hilo Uingereza. Man united pamoja na Wolverhampton Wanderers wapo katika kiwango kizuri. Wote wana soka la Kiingereza lenye kasi na kushambulia sana, uzuri zaidi hata upinzani kule si mkubwa. Kwani uwepo wa Shakhtar Donetsk, Inter Milan, Bayer Leverkusen hata Sevilla na Roma hawapo vizuri sana msimu huu, tuseme tu kuwa Inter ndiyo ataleta mtima nyongo kukwamisha kombe lisirudi Uingereza.
Kuna haja ya kuwaongelea Waingereza siyo kwa kuwa walitutawala aah aah la hasha hapana ligi yapo pia ni nzuri na inaangalika. Hata ndugu yetu Mbwana Samatta pia yupo huko pia, sasa inaachaje kututia wazimu inapovurunda kimataifa?


christopher
Msimu huu mambo hayajawaendea vizuri watu wa EPL kweny michuano ya ulaya
Fatina mfingi
Asnteh kwa taarifa meridianbet
Chiku
Maneno tumeyaelewa