Wachezaji wawili wa Simba Jean Baleke na Augustine Okrah wamepata majeraha katika mchezo wa kirafiki ambao klabu hiyo imekipiga na klabu ya Al Hilal na kutoka sare ya goli moja kwa moja.
Simba imekua ikiandamwa na majeraha sana msimu huu kwani ni kama wachezaji wake wanapishana kuingia kwenye majeraha. Baada ya Peter Banda na Moses Phiri kurejea uwanjani sasa ni Jean Baleke na Augustine Okrah wamepata majeraha huku ikiwa haijajulikana ni lini watarejea wachezaji hao.
Majeraha hayo yametokana na mchezo wa kirafiki baina ya wekundu wa msimbazi dhidi ya Al Hilal ya nchini Sudan, Ndipo nyota hao waliposhindwa kumaliza mchezo na kutolewa uwanjani baada ya kupata majeraha huku taarifa ya klabu ikisubiriwa ili kujua watakua nje kwa muda gani wachezaji hao.
Hii imekua ni hali ya hatari kwa klabu ya Simba baada ya kuumia kwa wachezaji wake wakati ambao wanaelekea kwenye michezo ya ligi ya mabingwa Afrika, Jean Baleke ambaye anaonekana ndio mshambuliaji namba moja wa klabu hiyo kwasasa inaweza kua pigo kubwa baada ya kupata majeraha.
Mshambuliaji Moses Phiri anaweza kua mbadala sahihi kwa Jean Baleke kwani raia huyo wa kimataifa wa Zambia ndio alikua mshambuliaji namba moja kwenye klabu hiyo kabla ya kuumia kwake, Hivo anaweza kurejea kwenye nafasi yake na kuwasaidia wekundu wa msimbazi kuelekea michuano ya ligi ya mabingwa Afrika.

