IKIWA juzi Jumatano alianza kazi rasmi ya kupandikiza mbinu zake kwenye kikosi cha Simba, kocha Abdelhack Benchikha raia wa Algeria, ujumbe pekee na mkubwa ambao aliwaachia Wanasimba ni kutuliza mioyo yao.
Benchikha ambaye amejiunga na timu hiyo akitokea kwenye klabu ya USM Alger ya kwao Algeria alisema, kwenye timu zote ambazo amewahi kuzifundisha hazijawahi kukosa mafanikio na Wanasimba wote wanapaswa kuwa na Imani naye.“Watu wanajua kazi yangu, mimi ni mtu ambaye napenda sana mafanikio kwenye kila timu ambayo nafundisha na nimekuwa na desturi hiyo kwa kuwa naelewa nini nahitajika kukifanya kwenye timu.“Mashabiki na wapenzi wa Simba, kubwa ninachohitaji kutoka kwao kwa sasa ni utulivu na wawe na imani na kazi yangu na wao wawe na imani pia na timu yao. Tutafanikiwa tukiwa na utulivu na ushirikiano,” alisema Benchikha.