KOCHA wa Simba, Juma Mgunda amesema kuwa anaufurahia muunganiko mzuri wa wachezaji wake katika eneo la kiungo linaloongozwa na Clatous Chama, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ na Pape Ousmane Sakho ambao kwa pamoja wameonyesha kuifanya Simba kuwa na makali.
Saido ni ingizo jipya ndani ya Simba ambapo baada ya kuungana na Chama na Sakho katika kikosi hiko kimeonekana kuwa na makali haswa katika eneo la ushambuliaji katika kutengeneza nafasi za kufunga na kufunga pia.
Mgunda alisema kuwa kwao ni furaha kuona timu imekuwa na muunganiko mzuri haswa katika eneo la kiungo ambalo limezidi kuwa bora kutokana na ongezeko la Sadio akishirikiana na wachezaji wengine ambao amewakuta kama Chama na Sakho.
“Kwa kweli tunamshukuru Mungu kutokana na kile ambacho kimeonekana ndani ya timu yetu, ongezeko la Saido ndani ya timu limetuongezea kitu kwa kushirikiana na wachezaji wengine ambao walikuwepo.
“Kuna muungukaniko mzuri ambao nimeuona kati yao Saido, Chama na Sakho kwenda katika eneo la ushambuliaji na wote wakiwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga, hiyo ni faida kubwa sana kwa upande wetu kwa kuwa tunakuwa na uhakika na nafasi za kufunga kutengenezwa lakini pia na upatikanaji wa mabao,” alisema Mgunda.