KOCHA mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kuwa anafurahia ushindani wa kila mchezaji katika timu yake huku akitamba kila mmoja atampanga kumtumia kutokana na aina ya timu atakayokutana nayo.
Kauli hiyo huenda ikawaingia hofu wapinzani wao wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Al Merrikh ya nchini Sudan. Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Septemba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Pele huko Kigari, Rwanda.Gamondi alisema kuwa ushindani ambao wanaounyesha wachezaji wake mazoezini ndio unampa jeuri ya kuchagua mchezaji yupi amtumie katika kila mchezo.
Gamondi alisema kuwa wachezaji wote wana uwezo wa kucheza mchezo wowote ulio mbele yao ukiwemo dhidi ya Al Merreikh, kikubwa mfumo atakaoingia nao watakapokutana nao ndio utaamua awatumie wachezaji gani, ili apate matokeo mazuri ya ugenini.
“Najua kabisa kila mpizani wetu tutakayekutana naye atakuwa amejiandaa kuhakikisha wanapata ushindi kwa kutumia michezo yetu iliyopita tuliyoicheza kuangalia ubora wetu.
“Lakini wafahamu kuwa mimi timu yangu ya msimu huu, sio ya kuitabiria ninapanga kikosi changu cha kwanza kutokana na aina ya timu ninayokwenda kukutana nayo.“Hiyo ni kutokana na usajili ambao tumeufanya msimu huu unanifanya niamue mchezaji gani wa kumtumia katika mchezo husika.
“Ushindani wa kila mchezaji kwa kuanzia safu ya ulinzi, kiungo na ushambuliaji ambayo imeonekana kufunga mabao mengi katika michezo michache tuliyoicheza msimu huu,” alisema Kocha huyo.