LICHA ya Yanga kuanza kwa kishindo cha ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya KMC lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema kuwa bado kidogo kikosi chake kuchanganya.
Yanga wameanza vyema kwenye ligi kuu ukiwa ni mchezo wao wa kwanza kwa ushindi wa mabao 5-0 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Azam Complex juzi Jumatano.
Kocha Gamondi alisema: “Nimefurahishwa na ushindi wa mabao 5 ambao timu tumeupata na hakika huu ni mwanzo wetu mzuri kwetu kuelekea katika kilele cha mafanikio ya ligi kuu.
“Kuhusu ubora niwapongeze wachezaji wangu lakini siwezi kusema kuwa wachezaji wamefikia asilimia 100 ya kile ambacho nilikuwa nimekitarajia bado kidogo.
“Wachezaji wangu haswa katika eneo la ushambuliaji bado halijakuwa katika ubora wa matumizi ya nafasi kwa ufasaha, naamini kila kitu kitakuwa sawa kwa kuwa ndio kwanza ni mwanzo wa msimu, tunaamini huko mbeleni tutaonyesha ubora mkubwa zaidi,” alisema kocha huyo.

