RAIS wa Klabu ya Yanga na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vilabu Afrika (ACA), ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Vilabu ya FIFA. Hersi Said, ameendelea kuthibitisha nafasi yake katika maendeleo ya soka la Afrika baada ya kushiriki mazungumzo muhimu kwenye kipindi cha kimataifa cha TransferRoom.

Katika mahojiano hayo, Hersi ameeleza kwa kina dhamira ya viongozi wa soka barani Afrika katika kujenga mifumo imara itakayohakikisha vipaji vya vijana vinalindwa, vinaendelezwa na kunufaisha vilabu pamoja na wachezaji kwa muda mrefu.
Mojawapo ya mada kuu iliyojadiliwa ni maendeleo na uhifadhi wa vipaji bora barani Afrika, ambapo amesisitiza umuhimu wa vilabu kuwekeza zaidi kwenye mifumo ya ndani badala ya kuuza vipaji mapema bila mipango endelevu.
Pia amegusia suala la kuunda njia imara kutoka shule na akademi za kufundisha mpira hadi timu za kwanza za vilabu, ameeleza kuwa mafanikio ya soka la kisasa yanategemea sana uwepo wa daraja linalowawezesha vijana kupanda hatua kwa hatua kwa misingi ya kitaalamu.
Hersi aliongeza kuwa kuwepo kwa miundombinu bora na sera sahihi kutawasaidia wachezaji vijana kupata mazingira salama ya kukua kiakili, kimwili na kiufundi kabla ya kukutana na changamoto za soka la ushindani wa juu.



