JUMA Mgunda, Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa mbinu pekee ambayo itawapa ubingwa wa Kombe la Azam Sports Federation lililopo mikononi mwa Yanga ni kupata matokeo kwenye mechi watakazocheza.
Juzi, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Eagle kwenye mchezo wa hatua ya raundi ya pili, Uwanja wa Mkapa.
Mgunda alisema kuwa malengo makubwa kwenye mashindano hayo ya Kombe la Shirikisho ni kupata ushindi kwenye mechi zao ambazo watacheza kwa ajili ya kubeba ubingwa mwishoni mwa mashindano.
“Unaona tumeanza kwa kupata ushindi mbele ya Eagle, sasa kinachoendelea ni kuendelea kupambana kwa mechi zijazo ili kupata matokeo chanya kwa kuwa ukipoteza mchezo safari inakuwa imeisha na sisi tunataka kufikia malengo yetu.
“Ikiwa utaniuliza kama tunahitaji ubingwa unadhani nini kitatokea kama tutapata matokeo chanya kwenye mechi zetu zote? Hii inaamanisha kwamba tutakuwa kwenye nafasi ya kutimiza malengo yetu na hii haitakuwa kazi nyepesi ni lazima tujitume na kutimiza majuku yetu,” alisema Mgunda.