KUNA vijana wangu kupitia kipindi cha Krosi Dongo kinachoruka Jumatatu hadi Ijumaa pale +255 Global Radio na Global TV Online, wana msemo wao kuwa Dabi ya Simba na Yanga inachezwa kila siku.
Maana yao ni kwamba, vurugu za mashabiki, wanachama na hata viongozi wa timu hizi, kila siku wanashindana kwenye mambo mbalimbali, iwe moja kwa moja kwa njia za kificho.
Lengo ni kutaka kuonekana wao ni bora kuliko wenzao. Hali hiyo imesambaa kama kirusi fulani cha ugonjwa hatari, kila mmoja sasa ameathirika na hilo limepelekea mvutano wao wa kila siku.Ipo wazi, hakuna jema ambalo Yanga watafanya kisha Simba wakapongeza kwa moyo mmoja. Na ikitokea wakapongeza, lazima kutakuwa na neon lakini ambalo linalenga kutoa kasoro fulani.
Ndiyo maana, hakuna shabiki wa Yanga hata mmoja ambaye anaweza akatoka mbele na kuwapongeza Simba kwa hatua kubwa waliyopiga kwenye mechi za kimataifa.
Simba kwa miaka mitano mfululizo, wameonesha kuwa inawezekana kuwapelekea pumzi ya moto wapinzani wa kiarabu, mfano ambao bado upo hai hadi sasa, ni mechi ya Misri baina yao na Al Ahly wikiendi iliyopita.
Watu wanabeza uwezo walionesha Simba pale Cairo International Stadium, watu wanahisi kama ilikuwa ni bahati mbaya Simba kutangulia kupata bao mbele ya Al Ahly na kucheza kwa mbinu ile.
Hayo ni mawazo ya kijinga kabisa na kutowapongeza na kuchagua kuwabeza Simba bado ni ujinga wa kiwango cha mwisho.
Siyo rahisi kutoka sare na Al Ahly wakiwa mbele ya mashabiki wao pale Misri, siyo rahisi kuwafunga au kupata bao pia, wakiwa kwenye mechi muhimu na wakiwa wanataka jambo lao.
Simba wameionesha Afrika na dunia kuwa inawezekana kabisa na ilikuwa kidogo tu waandike historia nyingine kubwa ya kuwatoa Al Ahly wakiwa kwao.
Ngoja niseme kitu. Ukitazama daraja la Al Ahly na kisha daraja la Simba kwenye makaratasi na uhalisia wa soka na kisha mtu akakwambie kuwa baina yao hakuna mshindi kwenye mechi mbili, basi wasifie Simba.
Waite Simba wanaume sababu wamekufa dhidi ya likitu likubwa kwao. Al Ahly wanamlipa Anthony Modeste zaidi ya shilingi za Tanzania milioni 350 na Percy Tau milioni 250 kwa pamoja ni zaidi ya milioni 600.
Wakati bajeti ya Simba kwenye mishahara ni wastani wa milioni 600 kwa mwezi ambapo ni sawa na wachezaji wawili tu wa Al Ahly. Maana yake ni kwamba Al Ahly wapo mbali kwa kila kitu mbele ya Simba.Mshahara wa Percy Tau wa mwezi mmoja ni mshahara wa Chama msimu mzima pale Simba, kwahiyo jasho la Chama limejawa na thamani sababu ni jasho la viwango.
Ukiona kina Zimbwe Jr wanaonekana wapo daraja moja na hawa watu wa Al Ahly jua wanavuja jasho la thamani tusiwatukane. Badala yake inapaswa tuwapongeze kwa kila kitu.
Simba, walikuwa wanashindana na timu mbili toka dunia tofauti, ni kama vile treni ya umeme na hii ambayo tumeizoea inafuka moshi. Al Ahly imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika uendeshaji barani Afrika na kuifanya iwe klabu ya karne.
Klabu iliyoshinda kwenye kila kitu kwenye mpira wa Afrika na hata dunia. Simba kwa bajeti yao ya mwaka wa fedha 2023/24 ni bilioni 23 na inalipa mishahara kwenye milioni 500 mpaka 600 ambazo ni kama bilioni 7 kwa msimu mzima.
Al Ahly inafanya hivyo kwa wachezaji wawili tu, ni jambo la kuwapongeza wachezaji Simba kwa kuvuja jasho kwa kiasi cha kuonekana wako kiwango sawa na Al Ahly.
Kubeza ni ujinga na inapaswa watu wajifunze kusifia kile kilichobora hata kama hawapendi.