Klabu ya Yanga Princess imeachana na kocha mkuu wa timu hiyo ya wanawake Edna Lema ‘Mourinho’ pamoja na kocha msaidizi Mohammed Hussein (Mmachinga).
Taarifa hii imetolewa na klabu hiyo na inaeleza kwamba, hivi karibuni klabu ya Yanga Princess itatoa taarifa kuhusiana na mbadala wa nafasi hizo.
Bado sababu za kuachwa kwa makocha hao wawili hazijawekwa wazi, lakini inadhaniwa kwamba matokeo mabaya inayoyapata klabu hiyo chini ya makocha hao, ni moja ya sababu ya kuvunjwa kwa mkataba wao.
Baada ya taarifa hiyo mashabiki mitandaoni walikuwa na maoni tofauti kuhusu uamuzi huo.
“Hii mmechelewa nafikiri wakati mwingine ukiona kitu hakifai ni bora kutafuta replacement kabla ligi haijaanza ingekua bora zaidi maana kuleta mtu mpya maana yake tunaanza upya kutafuta chemistry (muunganiko) ya/wa wachezaji kutafuta mpango mpya kuanza kusema mchezaji huyu hanifai haendani na mfumo sijui haya nyie ndo wajuaji tunategemea mtatafuta mbadala bora zaidi.”-Nasra Masi-Shabiki wa Yanga.