Ni suala la kihistoria kutokea katika klabu ya Manchester United kuwa na mtu atakayeshughulikia masuala ya ufundi; akipewa jina la Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu baada ya kumpa mtoto wa nyumbani Ole Gunnar mkataba wa kukinoa kikosi hicho. Sasa suala limekuja kwamba hawapo tayari kuendelea kushuhudia makosa ya usajili na wamefikia hatua ya kumtafuta myu atakayeshughulika na suala zima la ufundi.
Meneja aliyekwisha tangulia, Jose Mourinho alikuwa kinyume kabisa na suala hilo la kutaka kuwa na daraja hilo kati ya bodi ya klabu na ile ya wakufunzi. Na hadi ikapelekea Mourinho kutaka kuonana na Ed Woodward msimu uliopita ili kuliweka sawa hilo lisiweze kushika nafasi katika uongozi wake klabuni hapo.
Lakini kwa sasa kutokana na uteuzi wa kocha Solskjaer hivi karibuni klabu imeamua kuirejesha nafasi hiyo muhimu ili iweze kushikiliwa na kutumika vilivyo. Lengo likiwa ni kupata wachezaji wanaotakiwa na klabu kwa wakati sahihi na aina ya wachezaji wenye matumizi ndani ya klabu kuliko kuacha utawala ufanye masuala hayo nyeti zaidi ya kuripotiwa na safu hiyo itaanza rasmi kazi yake msimu wa 2019/20.
Pamoja na kwamba Solskjaer anategemea kuwa na usajili mzito msimu huu ili kujenga mapungufu ya kikosi chake lakini atatakiwa kwanza kuweka masuala yake safi na jopo hilo la wataalamu wa masuala ya kiufundi ili waweze kutoa maoni juu ya aina hiyo ya wachezaji wanaofaa kuchukuliwa kwa ajili ya kikosi cha kwanza.
Suala lililopo kwa sasa ni kwamba wao kama walimu wanaofundisha timu kazi yao ni kupendekeza majina tu kwa pale wanapoona panaweza kuwafaa lakini suala zima la kufuatilia juu ya nani aweze kuchukuliwa linabaki mikononi mwa dawati hilo la ufundi. Uzuri wa aina hizo za majukumu huchangia kuwepo kwa mazungumzo mazuri kati ya mihimili hiyo mitatu ya kikosi.
Solskjaer anaendelea kusema kwamba ni kweli kwamba soka kwa sasa limebadilika na mifumo inayoendesha soka hilo pia ni ya kipekee sio kama ile ya awali. Kwa misingi hiyo ya sasa yeye, Ed Woodward na Glazer watajikita zaidi kuangalia namna klabu inavyopaswa kwenda na kuendeshwa pekee. Na huo ndiyo mgawanyo wa majukumu ambao soka linataka kwenda kwa sasa na sio rahisi kuubadili.
Wanaotupiwa jicho kwa sasa ni Andrea Berta ambaye anafanya kazi na Atletico Madrid vilevile Fabio Paratici kutoka Juventus; japo bado kuna changamoto kwa sababu wanaangalia mtu ambaye ataendana na utaratibu wa klabu hiyo. Wengine ambao wanaangaliwa pia ni mkurugenzi wa klabu ya watoto ya klabu hiyo, Nicky Butt na mkuu wa kitengo cha maendeleo ya soka klabuni hapo ndugu John Murtough.

