Kiburi, jeuri na kujiona bora ndiyo maisha halisi ya mshambuliaji wa Kiitaliano mwenye asili ya Ghana, Mario Balotelli. Hapendi kujishusha, daima yeye hujiona yupo juu kuliko wengine, Wabongo tunasema kwamba anapenda kujimwambafai, kikubwa zaidi haambiliki. Katika umri wa miaka 29 Balotelli anachezea Brescia, timu ambayo inajikwamua isishuke daraja! Ingawaje amechaguliwa kuwa nahodha ila swali la kujiuliza ni sahihi Balotelli kuwa huku alipo? Na ilikuaje akafika huku? Kiwango kibovu au hana bahati?
Bila kupepesa macho jibu ni moja tu kuwa nidhamu imemfikisha huku alipo, Waswahili husema, “…mkaidi hafaidi hadi siku ya Iddi” naamini Balotelli anakula Iddi yake sasa, ila haijulikani ni Iddi ipi? Iddi ndogo au Iddi kubwa ya kuchinja.
Kama kuhusu kiwango hapo kila mtu atakataa, Balotelli ana kiwango cha juu, ni wale wafungaji wanaotumia nguvu nyingi kufumania nyavu (striker force). Anapiga mabao ya vichwa, ana mbio, anafunga kwa mipira ya faulo, ana uwezo wa kumiliki mpira na ana uwezo wa kukaba pale inapohitajika, ni mwepesi wa maamuzi. Kiujumla, Balotelli ana sifa zote za kuitwa mshambuliaji. Huwezi mlingamisha Balotelli na Lingard wa Man United au na Olivier Giroud wa Chelsea ila ajabu hawa wapo timu kubwa Ulaya, yeye yupo timu ndogo Italia. Tuseme ukweli hivi Balotelli anashindwa kupata namba Inter na AC Milan, Sevilla na Valencia au Everton na Tottenham? La hasha, anaweza ila tatizo ni kuwa haheshimu anachokifanya pengine hajui kuwa mpira ndiyo kazi yake.
Kama ni bahati Balotelli ana bahati kweli kweli maana kashachezea timu kubwa nyingi kweli kweli ikiwemo Inter na AC Milan, Man City pamoja na Liverpool ila wapi, aliondoshwa kwa nidhamu yake isiyokidhi vigezo. Siyo alisajiliwa hizo timu kwa mbeleko au connection aah aah alionesha kiwango hivyo makocha wengi wakatamani huduma yake, ajabu sasa. Mourinho aliiona joto ya jiwe kwa Balotelli 2009 na 2010 kipindi wapo Inter Milan. Balotelli hakuwa na heshima,
Mourinho alipojaribu kumkosoa kutokana na kiwango kibovu, Balotelli hakuwa nyuma alijibu mapigo kwa maneno ya hovyo, Mourinho aliishia kumtoa kwenye kikosi cha kwanza na kumhamisha hadi cha pili, hiyo ilikua 2009. Ajabu ni kuwa alipoomba msamaha Mourinho alimsamehe, wewe unafikiri angefanyaje wakati umuhimu wa Balotelli uwanjani unaonekana. Ila hakuishia hapo aliendeleza kiburi hadi kwa mashabiki kwani kuna kipindi alivua jezi na kuitupa uwanjani kuashiria kuwa amekerwa na mashabiki waliokuwa wanamzomea alipocheza chini ya kiwango dhidi ya Barcelona, Aprili 2010. Zanetti alinukuliwa akisema, “Mario must focus on doing what he can do on the pitch…” Akimaanisha kuwa Balotelli inabidi azingatie mambo ya uwanjani ila siyo vinginevyo. Mwishowe Inter wakamchoka na kutomuhitaji tena wakaamua kumuuza.
Man City wakaona kuwa huu ni muda wao muafaka wa kumchukua, Roberto Mancini kama kocha wa City alimsifia Balotelli kwa kusema kuwa ana umbo zuri na ataweza kuhimili mikiki mikiki ya ligi ya Uingereza. Hakuishia hapo akasema kuwa yale yote aliyokuwa anayafanya Balotelli ilikuwa ni utoto tu hivyo sasa atabadilika. Ni kama Balotelli alimuambia kuwa utabadilika wewe mie wala, hiyo ndiyo asili yangu. Kwanza anakupa raha kisha anakukera muda huo huo. Mancini alimuona Balotelli mwehu pale Balotelli alipotoa mpira nje kusudi alipojaribu kutaka kufunga bao kwa kisigino dhidi ya LA Galaxy, hili lilimfedhehesha Mancini akamtoa nje ya uwanja hapo hapo. Kisha akampa furaha pale alipotoa pasi ya bao iliyoisaidia City kuwafunga Queens Park Rangers na kutwaa kombe la Uingereza. Lakini akaendelea kujifanya mwamba!
Kiburi, mara kadi nyekundu, kukatwa mshahara kwa wiki mbili na kuanzisha taharuki kwenye vyombo vya habari haaaahaaahaa mashabiki wa Manchester United watakumbuka ule usemi wa “…why always me” alipowafunga na jezi yake kuwa na ujumbe huo. Mancini akaona isiwe taab bora yaishe akamuuza huko Uitaliano akiamini labda huko atatulia.
Alivyoenda AC Milan alikuwa moto kweli kweli mechi 13 goli 12 katika msimu wa 2012/13. Liverpool wakaona hapana tena wakiangalia Suarez kaondoka wakaamini basi atakuja kuziba pengo lake lakini wapi. Walau akiwa Liverpool kiwango kidogo kiliyumba, ila pia alikuwa mtovu wa adabu. Kwani aliwahi kutozwa faini ya pound 25 elfu, kufungiwa mechi moja kwa kosa la kuchapisha picha za kibaguzi kwenye mtandao ya kijamii. Mwishowe Liver wakamtoa AC Milan kwa mkopo wa muda mrefu napo hakufua dafu, alivyorudi Liverpool akakutana na Klopp ambaye alimuambia ukweli kuwa hamuhitaji kwenye kikosi chake.
Kufikia hapo Balotelli akaanza kuvuna alichokipanda, timu kubwa nyingi zilimkwepa sababu kuu ikiwa ni utovu wa nidhamu. Hata alipoenda Nice, Patrick Viera alikiona cha moto akajutia uamuzi wake wa kumsajili Balotelli. Mwishowe Balotelli amerudi Italia tena kwa dau la pound milioni 1 na nusu. Inajaabisha kwa kweli kwa kiwango cha Balotelli tena mwenye miaka 29 akacheze timu inayopambana kushuka daraja. Ila maisha ndivyo yalivyo hayakupi unachotaka. Waswahili husema ishi na watu uvae viatu haaahaaahaa ndiyo maana hatumshangai kumuona Balotelli akiwa peku.

