Klabu ya Chelsea bado inachechemea kunako ligi kuu ya Uingereza baada ya kukubali kichapo leo katika derby ya London dhidi ya klabu ya Westham United jioni ya leo.
Chelsea wanacheza mchezo wa pili bila kupata matokeo ya ushindi baada ya mchezo wa kwanza kutoka sare ya goli moja kwa moja, Lakini leo wamekubali kichapo cha mabao matatu kwa moja wakiwa ugenini katika dimba la London.
Mapema tu dakika ya 13 ya mchezo beki raia wa kimataifa wa Morocco Nayef Aguerd anaipatia bao la kuongoza klabu ya Westham kabla ya Carney Chukwuemeka kuisawazishia The Blues dakika ya 28, Lakini matajiri hao wa London walikua wana nafasi ya kuongoza kabla ya mapumziko kwani walipata mkwaju wa penati dakika ya 43 na kiungo Enzo akaukosa mkwaju huo.
Vijana wa Mauricio Pochettino walirudi kipindi cha pili wakionekana wakitafuta nafasi ya kusawazisha bao hilo walilotanguliwa, Lakini Westham waliendelea kuzuia kwa nidhamu na kufanya mashambulizi ya kushtukiza na yaliwalipa kwani dakika ya 53 ya mchezo Michael Antonio anafunga bao la pili katika mchezo huo.
Baada ya kufunga goli la pili Westham walilazimika kucheza pungufu baada ya beki wake Nayef Aguerd kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 67 ya mchezo, Huku ikionekana kama itakua nafasi kwa Chelsea kusawazisha lakini haikusaidia kwani kwenye dakika za nyongeza Westham wanapata penati Lucas Paqueta anaweka kambani na mchezo unamalizika kwa West Ham kuondoka na alama zote tatu.

