Rais wa klabu ya Barcelona, Josep Maria Bartomeu hana wasiwasi juu ya kusalia kwa Messi ndani ya kikosi chao katika msimu ujao huku kandarasi yake ikiwa inaelekea ukingoni kwa sasa. Mkataba wa mchezaji huyo upo katika hatua za mwisho kabisa huku ikionekana utaisha 2021 na Rais huyo anaamini kwamba mchezaji huyo atakubali tu kuongeza dili jipya la kuendelea kusalia kikosini hapo.
Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or amekuwa akihusishwa na kuihama klabu hiyo huku baadhi ya klabu zikiwemo Manchester City kuonekana kuvizia huduma yake. Lakini Bartomeu hana wasiwasi kwa kuona kwamba bado wana mahusiano mazuri na mchezaji huyo ambaye alijiunga na klabu hiyo tangu akiwa na miaka 13, hivyo klabuni hapo ni kama nyumbani kwake.
Messi ambaye mwezi Juni atasherehekea kumbukizi ya kuzaliwa kwake huku akitimiza miaka 32; alisaini kandarasi yake inayoelekea ukingoni mwaka 2017 na kizingiti cha kumnunua mchezaji huyo kilikuwa ni zaidi ya €700M kwa klabu yoyote itakayomuhitaji kwa namna yoyote ile. Na malipo ya kila wiki yanakadiriwa kupanda hadi $667,000. Sio kiasi kidogo kwa kumlipa mchezaji huyo na anastahili kwa aina ya uchezaji wake.
Mafanikio kwa kifupi
Mshambuliaji huyo wa Argentina na klabu ya Barcelona anaheshimika na kufahamika kama mchezaji bora wa muda wote na alianza kuingia katika ramani ya soka miaka ya 2004 ambapo miaka 14 baadaye, 2018 akiwa na klabu yake hiyo mwezi Machi alifunga goli lake la kihistoria mbele ya Atletico kwa kufikisha jumla ya magoli 600 katika maisha yake ya soka la kulipwa. Hiyo ni sehemu ya mafanikio aliyoyafikia kwa kipindi chake.
Dili zingine
Wachezaji wengine ambao mikataba yao ya kuendelea kusalia kikosini hapo inaelekea ukingoni wakiwemo Jordi Alba ambaye 2020 atakuwa anahitimisha kandarasi yake ya kusalia klabuni hapo na kwa mahitaji ya klabu bado wanahitaji kumshawishi aongeze kandarasi yake kuendelea kuhudumu nao kwa wakati uliopo kutokana na uwezo wake; japo hakuna majadiliano yanayoendelea kwa sasa juu ya kuongeza kandarasi hiyo.
Kwa sasa Bartomeu anakutana na kibarua kigumu baada ya mikataba ya wachezaji na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kuonekana inaelekea ukingoni na kukiwa na uhitaji wa kuongeza mikataba hiyo ili kurudisha morali ya wachezaji na viongozi wake ndani ya timu hiyo. Maana kila mmoja kwa wakati wake anataka kuangalia baadaye yake iko wapi ndani ya kikosi hicho endapo maafikiano yatafikiwa au ataruhusiwa kuachana na klabu hiyo.
Kocha Ernesto Valverde ataendelea kuhudumu klabuni hapo.


aisha
Ahsanteni kwa kutujuza