“Nilijua ni timu nzuri, lakini nataka Messi anyanyue kombe, amesema nyota wa AC Milan”- Zlatan Ibrahimovic
Tuko kwenye nusu fainali ya Kombe la Dunia la FIFA nchini Qatar ambayo inamaanisha kuwa mashindano hayo yanakaribia mwisho wake. Morocco imekuwa timu ya kushangaza kwa wengi lakini sio kwa nyota wa AC Milan Zlatan Ibrahimovic.
Mshambuliaji huyo mashuhuri wa Sweden yuko na mabingwa hao wa Italia huko Dubai kwenye mazoezi ya hali ya hewa ya joto kabla ligi kurejea mwishoni mwa mwezi Disemba, anasema alijua Morocco ingefika mbali katika mashindano hayo.
“Sidhani kama ni jambo la kushangaza kwamba Morocco imefanya vyema katika Kombe la Dunia,” anasema mchezaji huyo wa miaka 41. “Nilijua walikuwa wazuri kabla ya Kombe la Dunia lakini ni wazi wakati wa mashindano chochote kinaweza kutokea.
“Ni timu nzuri, ni taifa zuri na watu wanafurahia maajabu ya aina hii kwa sababu washindani wanaposhinda huwa haishangazi. Ngoja tuone kama wanaweza kufika fainali.”
Ibrahimovic, ambaye aliisaidia AC Milan kushinda taji la Serie A msimu uliopita huku akicheza na jeraha baya la goti anahisi Ufaransa ina nafasi nzuri ya kuhifadhi taji hilo. “Ni wazuri, walishinda Kombe la Dunia mwaka 2018 wakiwa wadogo, wamezeeka kidogo sasa na wako imara.
“Pia sishangai Croatia wako katika nusu fainali kwa sababu walikuwa kwenye fainali kwenye Kombe la Dunia lililopita. Lakini nadhani tayari imeandikwa nani atashinda – na unajua ninamaanisha nani. Nadhani Messi atanyanyua kombe kwa ajili ya Argentina.”
Majeraha ya Ibrahimovic yanaendelea vizuri lakini hatashiriki katika mechi zijazo za AC Milan za Dubai Super Cup dhidi ya Arsenal usiku wa leo au Liverpool Ijumaa. Mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona anasema hana uhakika ni lini atarejea kucheza.
“Ninafuata utaratibu ninaohitaji kufuata na kila siku inazidi kuwa bora lakini ni mchakato mrefu na tulijua itakuwa. Jambo kuu ni kuwa na subira. Hakuna tarehe ninapotakiwa kurudi. Ni kuhusu kujisikia vizuri katika afya yako, kisha hatua ya pili ni kucheza soka.”
Alikuwa akichoma sindano za kupunguza maumivu msimu uliopita alipokuwa akiiongoza timu kupata ushindi na anakiri kuwa ilikuwa hatari na ingeweza kufanya jeraha kuwa baya zaidi.
“Kila nilipoweka mguu wangu uwanjani nilijua kungekuwa na matokeo lakini sijutii. Ningefanya tena kwa sababu mawazo yangu ni hayo. Niko kwenye mchezo wa kushinda, nafanya kila kitu ili kushinda, kusaidia wenzangu kushinda.
“Nilijua sikuwa sawa kwa asilimia 100 lakini mwishowe tulishinda, lakini sasa ninalipa nilichopitia kwa hiyo tuseme kila kombe lina gharama yake na gharama hii ilikuwa goti langu.”