Nyota wa Kitanzania na mchezaji wa timu ya taifa la Tanzania, Mbwana Samatta anayekipiga nchini Ubelgiji na klabu ya Genk amefikia mafanikio makubwa ambayo kwa hakika hakuna Mtanzania mwingine aliwahi kuyafikia ndani ya maisha ya soka tangu waanze kucheza soka la kimataifa.
Ni dalili njema sana kwa soka la nchi hii hususan pale mafanikio ya aina hii yanapokuwa yanafikiwa na wachezaji ambao ni wazawa kwa nchi za ukanda huu wa Afrika Mashariki. Nafasi hiyo imekuja baada ya timu yao kunyanyua kombe la ligi baada ya kuwazidi alama Club Brugge ambao walikuwa wapinzani wao wakubwa msimu huu.
Ushindi wa kombe hilo kwa klabu hiyo ni wa nne katika historia na ni wa kwanza tangu mwaka 2011 kwa sababu kwa kipindi chote hicho hawajaweza kabisa kushinda taji. Mataji mengine waliyowahi kushinda katika ligi ni yale ya 1998/99, 2001/01 na 2010/11 na hili la msimu huu ndilo la nne.
Mbali na ushindi huo wa kombe la ligi pia, wamechukua makombe mbalimbali ndani ya taifa hilo katika msimu wa 2008/09 na 2012/13. Hatua kama waliyoifikia msimu huu waliwahi kuifikia msimu wa 2013 ambapo walifanikiwa kupenya kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa.
Nyota huyo wa zamani wa klabu ya Wekundu wa Msimbazi (Simba) amekuwa katika msimu wa pekee kwenye ligi hiyo akio!nesha ukomavu wa pekee sana ndani ya ligi hiyo hadi kuwavuta vigogo mbalimbali kushawishika. Alijiunga na KRC Genk 2017 akitokea kwa miamba wa soka wa Congo, TP Mazembe.
Mbali na kushinda taji hilo la ligi na kupata nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano ya klabu bingwa msimu ujao amefanikiwa kuchukua tuzo mbalimbali zilizotokana na uwezo wake mkubwa sana ikiwemo ile ya Ebony Shoe: ambayo ni kiatu anachopewa mchezaji aliyefanya vizuri ndani ya ligi hiyo akiwa amevunja rekodi ya Moumouni Dagano wa Burkina Faso mwaka 2002. Hivyo ni mchezaji wa tatu kushinda tuzo hiyo.
Pia, ameongoza timu yake kwa kufunga magoli mengi zaidi ndani ya ligi hiyo na kufanikiwa kuchukua kiatu cha mfungaji bora mara baada ya kufikisha magoli 23 ambayo hayajafikiwa na nyota mwingine. Kwake hilo ni jambo jingine la kihistoria.
Tuzidi kumtakia mafanikio zaidi anapoipeperusha vyema bendera ya taifa lake.


Isha
safi sana mtazania anayejituma
Mariam mtandama
Safi