Klabu za Chelsea, Manchester City zimefanikiwa kushinda michezo yao ya leo katika ligi kuu Uingereza huku klabu ya Leicester ikiendelea kuchechemea.
Chelsea iliokua nyumbani katika dimba la Stamford Bridge imefanikiwa kupata alama tatu muhimu na magoli matatu baada ya kushinda magoli matatu kwa bila dhidi ya Wolverhampton ikiwa ni mara ya kwanza toka 2019 kuifunga timu hiyo katika ligi kuu ya Uingereza.
Magoli ya Kai Havertz,Christian Pulisic, pamoja na Armando Broja yalitosha kuwazima mbwa mwetu darajani na kuwafanya Chelsea kusogea hadi nafasi ya nne na alama zao 16.
Manchester city wao wameigaragaza klabu ya Southampton kwa mabao manne kwa bila magoli ya Joao Cancelo,Phil Foden, Riyad Mahrez huku Earling Haaland akiendeleza makali yake baada ya kufunga bao la nne la mchezo huo huku City wakikwea kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha alama 23.
Klabu ya Leicester City yenyewe ikishindwa kutamba mbele ya Afc Bournemouth baada ya kufungwa mabao mawili kwa moja katika dimba la vitality Stadium. Leicester ambao waliicharaza Nottingham Forest kwa mabao manne kwa bila katikati mwa wiki leo wameshindwa kutamba na kuambulia kipigo.

