“NI Ijumaa murua, Ijumaa ya kihistoria karibu kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika fainali ya kwanza katika historia kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam chini ya TFF ya Karia.”
Hii siyo ndoto tena bali ni historia mpya ambayo itakwenda kuandikwa mwaka 2027 baada ya mapacha wa Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda kushinda zabuni ya kuwa wenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu mataifa haya kuanzishwa.
Wazo la kuwa wenyeji wa michuano ya Afcon lilianza mwaka 2019 baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano ya Afcon kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 michuano ambayo ilifanyika kwa ufanisi mkubwa na ndipo wazo hili lilikuja.
Kutokana na uchache wa miundombinu hususan viwanja tukaona si haba kuwashirikisha majirani zetu Kenya na Uganda ambao waliungana nasi bila mgagaziko wowote na rasmi tutaandaa michuano hii mikubwa barani Afrika kwa upande wa timu za taifa.
Waswahili wana msemo wao kuwa mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Moja ya watu ambao wameifanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na Serikali yetu tukufu ni mwanandamu kutoka Tanga.
Huyu si mwingine ni Wallace John Karia Rais wa TFF ambaye tangu ameingia madarakani tumeshuhudia mageuzi makubwa kwenye soka katika ngazi zote kuanzia timu za vijana, timu za wanawake na timu za wakubwa (Taifa Stars na Twiga Stars).
TFF ya Rais Karia imeendelea kuacha vitendo zaidi viongee kuliko maneno kwa mara ya kwanza. Ligi za madaraja ya chini kwa maana ya Championship na First League zimepata udhamini mnono, Ligi Kuu Bara ikizidi kuchanjambuga.
Huku tukishuhudia mafanikio makubwa kwa timu zetu za wasichana na timu za vijana kwenye michuano ya CECAFA na COSAFA huku Twiga Stars ikiwa imebakisha hatua moja mbele kufuzu michuano ya AFCON kwa wanawake.
Nitawahadithia wajukuu zangu kuwa nimewahi kuishuhudia TFF bora kwenye kizazi changu na TFF hiyo ilikuwa inaongozwa na Wallace Karia, kwenye kila taasisi mapungufu hayakosekani jambo ambalo linanisikitisha ni kuwa asilimia kubwa ya sisi tunaojiita watu wa soka tumechagua upande wa mabaya zaidi na kuyafumbia macho yale mema ya TFF ya Rais Karia.
Yale machozi aliyomwaga pale Kairo wakati tunatangazwa kuwa wenyeji wa michuano ya AFCON yalikuwa na maana kubwa maana bibi yangu aliwahi kuniambia mwanaume halii ovyo na ukiona analia ujue kuna sumu kubwa kaitoa.
Machozi ya Karia yalikuwa na maana kubwa kuwa licha ya mikuki anayopigwa lakini yeye kachagua kuupeleka mpira wa Tanzania nchi ya ahadi yenye maziwa na asali.
Hongera Afrika Mashariki, hongera TFF, hongera Wallace Karia wewe ni alama isiyofutika kwenye soka letu. Natamani sanamu lako lijengwe pale Karume ili iwe kumbukumbu kuwa tuliwahi kuwa na Rais bora wa Shirikisho ambaye ni Wallace Karia. Karibu Temeke

