Klabu ya Yanga imekubali kichapo tena katika mchezo wa ligi kuu ya NBC baada ya kufungwa mabao mawili kwa moja na klabu ya Ihefu ya Jijini Mbeya katika mchezo uliopigwa jijini humo leo.
Ihefu wameweza kuendeleza rekodi yao katika ligi kuu dhidi ya mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya NBC baada ya kuwatembezea kichapo kwa mara nyingine wakiwa katika dimba lao la Highland Estate.Klabu ya Yanga ndio walikua wa kwanza kupata bao mapema kabisa dakika ya nne ya mchezo huo, Lakini Ihefu walionesha ukomavu na kuhakikisha wanasawazisha bao hilo baada ya kusawazisha bao dakika ya 41 ya mchezo na mchezo kwenda mapumziko kwa bao moja kwa moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo kila timu ilihitaji kupata bao la kuongoza mchezo huo, Ihefu ndio walioweza kupata bao la pili mchezo huo baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza dakika ya 66 na Charles Ilanfya kuweka bao la pili kimiani.Mchezo uliondelea kwa kosa kosa nyingi kwa pande zote mbili ambapo Yanga ndio walionekana kutafuta bao la kusawazisha zaidi, Lakini mchezo uliweza kumalizika kwa Ihefu kuondoka na alama zote tatu na huku wakionesha ubora mkubwa haswa safu yao ya ulinzi.