Real Madrid wanafikiria kupata wachezaji watakaoleta chachu mpya ndani ya kikosi chao mbele ya kocha wao aliyepata nafasi ya kukinoa kikosi hicho kwa awamu ya pili, Varane kwa sasa anaangalia namna atakavyoweza kujiunga na vilabu vingine endapo atachukua maamuzi ya kuingia sokoni kwa sasa.
Hii inakuja baada ya kupata mafanikio makubwa na klabu hiyo ndani ya misimu nane yenye mafanikio makubwa sana akiwa amefanikiwa kushinda vikombe viwili vya ligi, makombe ya klabu bingwa barani Ulaya na yale ya klabu bingwa ya dunia. Hayo ni mafanikio makubwa sana kwa mlinzi huyo raia wa Ufaransa mwenye historia kubwa ndani ya jiji hilo.
Mchezaji huyo anayetazamiwa kufikisha miaka 26 hivi karibuni hana wasiwasi kuhama klabuni hapo kutokana na uwezo wake na aina ya mafanikio ambayo ameyapata ndani ya klabu hiyo na hata klabu nyingine hawawezi kuhofia nafasi yake kutua kikosi chochote atakachopata nafasi ya kujiunga nacho.
Mara nyingi wachezaji wanapokuwa katika viwango vya aina yake wanapojiunga na klabu nyingine mara nyingi hushuka kwenye viwango vyao na kuwafanya kupotea kabisa kihistoria. Kwa Varane ndani ya kikosi hicho ni mchezaji ambaye amefanikiwa kuwa beki bora duniani akiwa katika kikosi cha timu yake ya taifa pia katika klabu yake ya Real Madrid. Kinachompa jeuri mchezaji huyo ni kwamba klabu kubwa barani Ulaya zinamhitaji na baadhi yake ni:
Manchester City, kwa kuangalia kikosi chao bado wanahitaji kuwa na aina ya walinzi kama hawa ili kujiimarisha zaidi. Hii ni kutokana na uwepo wa wachezaji kama Aymeric Laporte ambaye amekuwa na kiwango kisichobadilika mara kwa mara lakini uwepo wa wengine kama Otamendi ambaye umri umesogea na Vincent ambaye umri wake umesonga mbele kwa sasa. Hivyo wana uwezekano wa kumfanya atue.
Paris Saint-Germain, hii inatokana na umri wa mlinzi wao wanayemtegemea, Thiago Silva kuwa kwa sasa umepanda sana kiasi ambacho kinahisiwa kwamba uwezo unaweza kuendelea kushuka kiasi cha kuhitaji mchezaji ambaye ataweza kuwa mbadala wake na mwenye uwezo wa juu na wasifu mkubwa kama wake.
Liverpool, kwa sasa wanaonekana kuwa katika kampeni ya kupata walinzi ambao watasaidia kikosi hicho kufanya vizuri zaidi ya hivi sasa. Wanaangalia mlinzi mwenye wasifu wa aina yake ili aweze kufanya kazi na Van Dijk kwenye michuano mikubwa wanayoshiriki kwa sasa.
Klabu nyingine zinazoonekana kuthamini uwezo wa mlinzi huyo ni Juventus, Bayern Munich na Manchester United ambao wanathamini uwezo wa mchezaji huyo na kuhitaji huduma yake, hata akiingia sokoni watakuwa katika harakati za kutumia mawakala wao kumnasa. Japo ujio wa Zidane unaweza kumfanya mchezaji huyo abadili maamuzi yake hayo.


Furahav
Varane hata akiondoka sawa,mana kashachukua vikombe vyote.