Kasi ya kukifukuzia kiatu cha dhahabu imekuwa sio ya kawaida kutokana na uchekaji na nyavu ulivyokuwa na kasi kubwa ndani ya ligi kuu ya Uingereza. Kwa sasa kila mchezaji anajitahidi kwa nafasi yake kujaribu kusuka historia ndani ya ligi hiyo ili aweze kukivaa kiatu hicho pale ligi hiyo itakapokuwa inamalizika.
Machester City na Liverpool hawana wasiwasi kabisa juu ya ushiriki wao kwenye michuano yote mikubwa ya mbeleni kutokana na alama walizonazo kileleni mwa ligi hiyo; kazi inabaki kwa wengine kama Manchester United, Chelsea na Arsenal ambao wana jukumu zito la kuhakikisha wanachukua nafasi ya nne ili kujiwekea nafasi yao kushiriki michuano hiyo mikubwa Ulaya.
Huku kila klabu ikiangalia juu ya nini wakifanye kwa sasa huku wakitafuta kuwekeza alama zitakazowapa angalau ubingwa au kujiweka katika nafasi nzuri baadhi ya wachezaji wao wapo katika kinyang’anyiro cha kupata kiatu cha dhahabu ambacho hukabidhiwa yule aliyeonesha uwezo mkubwa wa kufumania nyavu zaidi ya wengine.
Mbio hizo kwa msimu huu zimekuwa na kasi ya ajabu huku kukiwa na wachezaji zaidi ya watano wakipigania nafasi hiyo nyeti sana ndani ya ligi husika. Baadhi ya wachezaji waliopo katika kinyang’anyiro hicho ni Sergio Arguero, Mohamed Salah, Hary Kane, Sadio Mane, Aubameyang na Raheem Sterling.
Aguero ni kinara katika takwimu hizo akiwa na jumla ya magoli 18, akifuatiwa na Salah mwenye 17, Kane 17, Mane 17, Aubameyang 17 na Sterling 15. Wote hao wanaangalia uwezekano wa kupata nafasi ya kushinda kiatu hicho. Wengi wao ni wachezaji ambao klabu zao zipo katika nafasi za kinyang’anyiro cha ubingwa.
Msimu uliopita Salah alitwaa kiatu hicho kwa kumtupa Kane kwenye ushindani huo ambapo waliweza kutofautiana idadi ya magoli mawili pekee huku Salah akimaliza na magoli 32 na Kane akimaliza na magoli 30. Raia huyo wa Misri alikuwa kwenye kiwango bora zaidi msimu uliopita kitu ambacho ni tofauti kidogo na msimu huu akiwa kidogo anasuasua kupata magoli uwanjani kitu ambacho kimeanza tayari kuleta wasiwasi kwamba kiwango hicho yawezekana kisijirudie.
Tofauti na msimu uliopita ni kwamba Salah kwa msimu huu hajapata bahati ya kufumania nyavu katika mechi zake saba alizocheza kwenye michuano yote. Kitu ambacho kinafanya awe nyuma ya kinara wa ligi hiyo Aguero. Pia, idadi ya magoli msimu huu inaweza ikashindwa kuivunja rekodi ya mwaka jana kama ukame wa magoli utaendelea.
Kwa sababu ligi bado inaendelea kushika kasi ya pekee ni dhahiri kwamba tutashuhudia magoli mengi yakiendelea kumiminika ndani ya ligi hiyo katika msimu huu huku wachezaji hao wakiendelea kuchuana vikali kuhakikisha wanabakiza viatu hivyo ndani ya makabati yao ikiwa kama sehemu ya historia nzuri.


aisha
Kweli kiatu cha dhahabu sio powa
Nasra
Hongera sana kupata kiatu cha dhahabu