Klabu ya Real Madrid ipo katika kipindi kizito cha kuangalia aina ya wachezaji ambao wataisaidia klabu hiyo kurejesha heshima ya kunyanyua mataji. Wakiwa katika hatua hiyo lazima waangalie sokoni kuna aina gani ya wachezaji ambao watawafaa kwa nafasi fulani ili kuleta ushindani.
Miongoni mwa wachezaji ambao klabu hiyo inawahitaji ni Eriksen ambaye anakipiga chini ya Pochettino kwenye klabu ya Tottenham. Mchezaji huyo, kwa nafasi kubwa, amekuwa injini kubwa katika eneo la katikakati la kikosi hicho kwa kuwa na jicho kubwa lililowafanya kupata mafanikio ya haraka yaliyowashangaza wengi.
PSG nao wanaangalia wachezaji wa aina yake ambao wanajua maana halisi ya kuipigania timu hivyo, sasa wanaonekana kuingia sokoni kuwapa upinzani Madrid. Wote wawili hawa wana pesa zinazoweza kumshawishi lakini kwa mchezaji ambaye anaangalia mafanikio zaidi lazima ataweza kuchagua Madrid ambao hata historia yao inawabeba zaidi.
Madrid tayari wamefanikiwa kushusha silaha zao kadhaa kwa ajili ya msimu ujao na bado wapo sokoni kusajili nyota wengine zaidi ambao watakuwa msaada hapo. Kikubwa matajiri wa Madrid wao wanaonesha zaidi utendaji kuliko maneno hivyo kwa mchezaji wanayemhitaji haiwapi shida kabisa kumega fungu la pesa na kumfukuzia.
Nyota huyo wa miaka 27 amekiri wazi kwamba mbali ya kuwa na furaha ndani ya kikosi hicho cha Spurs lakini bado anaamini hajafikia pale anapotamani kufikia na kama akiweza kuikamilisha furaha yake basi atakuwa tayari kujiunga na klabu ambayo inaangalia mafanikio zaidi na hilo ndilo linaloweza kumuondoa kikosini hapo ili aweze kujaribu radha nyingine ya ushindani.
Taarifa hizo za kutimka kikosini hapo sio rafiki kwa kocha na mashabiki wa kikosi hicho kutokana na namna mchezaji huyo alivyo msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Spurs. Katika mashindano ambayo amekuwa akicheza hii ikiwa katika timu ya taifa na hata klabu yake amekuwa nguzo ya aina yake na amechangia kwa asilimia kubwa mafanikio ya klabu hiyo.
Mbali na uhitaji wao, Madrid wametenga kitita cha £130M ili kufukuzia saini yake wakati PSG nao wakionekana kumuhitaji mchezaji huyo kwa gharama kama hiyo japo wao wameweka mezani majina mawili likiwemo la Draxler na Eriksen ambao wanahisi watakuwa matunda ya mafanikio ndani ya klabu yao.


Povel
Kuna nn tena