Kwa miaka mingi utamu na uzuri wa soka umekuwa ukishuhudia majina mawili yanayozungumziwa sana kwenye vyombo vya habari, mashabiki na hata maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ya watu wanaopenda na wasiopenda soka. Kwa maana hiyo wawili hao walifanikiwa kuliteka soka kwa upande mkubwa sana.
Lakini, umri wa wawili hao kuendelea kuwika kama ilivyokuwa hapo awali umesogea, jambo ambalo kwa hakika linawafanya wengine kuikaribia nafasi hiyo ili kuwa gumzo zaidi ya ilivyokuwa kwa wawili hao katika miaka yote ambayo waliweza kushika nafasi hiyo ya juu.
Haizuiliki kabisa kwa nafasi yao lakini upinzani wao ulianza kushuka pale mmoja wao alipoihama ligi ambayo iliwaweka wawili hao kwa ukaribu na pindi wanapokutana kila mmoja alikuwa anawaza namna gani anaenda kuonesha ubora wake wa kufumania nyavu mbele ya mwenzake ili kujenga historia.
Baada ya kizazi cha wawili hao haina maana kwamba basi na safari ya soka kushika nafasi ya ushindani imekomea hapo; ni kwamba kuna wengine lazima watashika nafasi hiyo na vichwa vya habari ili kuonesha ubora wao. Wafuatao wanaweza kushika nafasi hiyo kama watatambua nafasi zao kwenye klabu zao:
Neymar – Eden Hazard, wawili hawa tayari wamejitambulisha kwamba wao ni zao bora kabisa ndani ya soka, hivyo kama wataendelea kukomaa kadri siku zinavyozidi kusogea kwa hakika watafanya makubwa na kuwa kama ilivyokuwa kwa wawili hao ambao wameweka heshima ndani ya soka.
Kylian Mbappe – Marcus Rashford, hawa wote uwezo wao sio wa kubezwa; kasi, maarifa na uwezo wa kupambana na nyavu ni vitu ambavyo wamejaaliwa kadri siku zinavyosogea wanazidi kuwa bora na kujijenga zaidi. Kwa hakika ni kizazi cha kutumainiwa sana kwa siku za usoni kwenye upande huu wa soka.
Jadon Sancho – Joao Felix, Manchester City walipoteza tunu kubwa kwa kuipeleka Dortmund na amekuwa na kiwango cha pekee sana. Ameanza kutabiriwa makubwa akilinganishwa uwezo wake na nyota huyo wa Benfica kwamba taa za kufanya vizuri zinawaangaza na huenda wakaja kuwa na historia imara sana.
Ousmane Dembele – Vinicius Junior, hawa tayari wameanza kuonesha njia inayotabiriwa kuja kutokea. Uwezo wa kila mmoja hata wanapokuwa uwanjani tayari ni kipimo tosha kwamba watakuja kuwa na historia isiyozuilika kwa siku za usoni na ni kizazi halisi cha Messi na Ronaldo ambacho kitatumika kama mrejesho wa wawili hao kwenye maisha ya soka ambayo waliyaishi na matunda waliyoacha.


Janeflora malisa
Nice