Wawili hawa ni mahasimu wakubwa wa ndondi duniani. Kila mmoja anaheshimu uwezo wa mwenzake kutokana na pambano lao lililopita kuwa lenye ushindani mkubwa na lililoibua hisia za aina yake kwa mashabiki wa mchezo huo. Ambapo mshindi alipatikana kwa maamzi ya alama [pointi] tu ambapo ilionekana wamezidiana vitu vichache.
Hivi juzi wawili hao walikutana bila kujua kama wote walikuwepo katika eneo lile, ambapo mechi ya mpira wa kikapu ilikuwa inaendelea. Pacquiao na Mayweather wote walihudhuria mechi hiyo ya kikapu kati ya LA Clippers dhidi ya Charlotte Hornets katika viwanja vya Staples Center kule Marekani [ Los Angels].
Kama ilivyo kwa binadamu Pacquiao alimfuata mshindani wake na kumsalimia huku kelele za mashabiki zikiwa juu; wakishangilia kukutana kwa wawili hao katika viwanja vile. Ndani yake fununu za wawili hao kurudi ulingoni zikiwa zimechukua nafasi yake. Mashabiki wana yao juu ya kutaka wawili hao waweze kukutana tena kwa awamu nyingine, japo katika pambano lao la mwanzo Mayweather baada ya ushindi ule 2015 alitangaza kustaafu kupanda ulingoni tena.
Kwa sasa Mfilipino huyo anajiandaa na pambano lake kati yake na mkongwe wa masumbwi Adrien Broner litakalofanyika Januari, 19 huku akiwa anasisitiza kwamba pambano hilo linategemewa kuwa ni gumu sana upande wake kwa sababu mpinzani wake ni mkongwe na mwenye mbinu nyingi juu ya mchezo huo wa masumbwi.
Na kama mambo yataenda sawa katika pambano hilo la mwanzo la Mfilipino huyo basi mwezi June tutegemee kuona pambano jingine la kurudiana kati ya wawili hao waliojenga historia kubwa duniani hadi sasa.
Japo Pacquiao anajaribu kufuta uvumi wa pambano hilo la kurudiana na mpinzani wake mkubwa, lakini kwake yeye anasema pambano lake na Bronee ndilo analolipa kipaumbele zaidi kwa sasa, kwa sababu ndilo lililokwenye kalenda yake na ndilo analojifua kwa ajili ya kukutana na huyo mpinzani wake hivyo haoni sababu za kuzungumzia sana juu ya pambano ambalo bado halijakaliwa ili kufikia makubaliano.
Siku zote lisemwalo lipo, pambano hili haliwezi kuzuilika kutokana na ushawishi mkubwa unaofanywa na mashabiki pamoja na vyombo vya habari duniani. Ni vigumu kufuta taswira za pambano lile la kwanza vichwani mwao; kitu ambacho lazima kiwekewe uzito wa pekee ni wawili hawa kukaa upya mezani na kupanga tena kama waweze kurudiana kutokana na kila mmoja kutomwogopa mwenzake. Uvumi wa mashabiki hauzimwi kwa maneno tu bali kwa vitendo ili kudhihirisha ubora wa wanachokiamini vichwani mwao.

