UONGOZI wa Simba, umeweka wazi kuwa njia, pekee itakayowapeleka katika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ni kushinda mechi zote za nyumbani ili kurejesha hali ya kujiamini zaidi.
Ipo wazi kuwa baada ya kucheza mechi tatu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo ni dakika 270, Simba haijaambulia ushindi.
Ilipoteza mchezo wake uliopita dhidi ya Wydad Casablanca kwa bao 1-0, iliambulia sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya ASEC Mimosas na Jwaneng Galaxy 0-0 Simba.Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa kazi ni kubwa kutafuta ushindi kimataifa, lakini inawezekana kufanikisha malengo yao.
“Kazi ni kubwa katika mechi ambazo tunacheza kwenye anga la kimataifa tunatambua haitakuwa rahisi lakini ili tufanikishe malengo yetu lazima tuanze kushinda kwenye mechi zetu za nyumbani.“Hatua ya robo fainali ni malengo yetu na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mechi zetu zote, tulianza kwa kupoteza pointi mchezo wa kwanza nyumbani lakini tuna nafasi ya kupata pointi kwenye mechi zilizopo,” alisema Ahmed Ally.