Hatimaye droo ya michuano ya klabu bingwa na kombe la shirikisho imetoka hapo jana ambapo kwa upande wa klabu bingwa mwakilishi pekee Simba kutoka Tanzania amepangiwa Wydad Casablanca.

Ikumbukwe kuwa Simba ametoka kumaliza wa pili kwenye kundi ambalo kulikuwa na timu kutoka Morocco ambayo ni Raja Casablanca na sasa tena wamepewa mpinzani mkubwa wa Raja ambae ni Wydad.
Wydad ndiye bingwa mtetezi wa kombe hili la klabu bingwa ambalo alilichukua baada ya kumtandika Al Ahly kwenye fainali waliyocheza mwaka jana na sasa amefika hatua ya robo fainali.
Wydad kwenye ligi ya Morocco Botola Pro anashikilia nafasi ya pili akiwa na pointi zake 43 baada yakucheza michezo yake 21, ameshinda michezo yake 12, sare 7, na kapoteza michezo miwili pekee.

Wakati Simba naye kwenye Ligi kuu ya NBC yupo nafasi ya pili akiwa na pointi zake 57, baada ya kucheza michezo yake 24, ushindi mara 17, sare 6 na kupoteza mara 1 pekee hadi sasa.
Michuano hiyo mkondo wa kwanza itapigwa kuanzia tarehe 21-22 mwezi April, na mechi za mkondo wa pili zitapigwa kuanzia tarehe 28-29 mwezi huo huo kujua nani anakwenda Nusu Fainali.

