Imeshuhudiwa mechi kali na ya aina yake katika ligi kuu ya Uingereza jana ambapo miamba wa soka nchini humo, Manchester United na Chelsea wakiumana kwa soka la kuvutia na kuonesha ukomavu wa aina yake jambo ambalo liliwaburudisha mashabiki wa soka duniani kote.
Mpira ulianza kwa kasi ya ajabu na kila timu ikitafuta nafasi ya kuonesha kiwango chake mbele ya mwenzake jambo ambalo lilifanya mechi iweze kuvutia sana. Chelsea walianza kwa kasi ya ajabu wakipiga pasi nyingi ambazo zilionekana kila klabu ilikuwa inamuona mwenzake vizuri japo walikosa umakini wanapofika eneo la kushambulia mbele ya walinzi wa United walioonekana kuiva sana na kucheza kwa kujiamini.
Haikuchukua muda pale safu ya ulinzi ya Chelsea ilipocheza makosa na kuwaacha washambuliaji wa United, Rashford na Martial kugusiana mpira jambo lililopelekea kupatikana kwa mpira wa adhabu ndani ya eneo la hatari la Chelsea na muamuzi kuamuru penati kupigwa ndipo Rashford akafanikiwa kuwaandikia wenyeji hao goli la kuongoza.
Chelsea wakiwa na ari ya ajabu pamoja na kikosi chake kilichosheheni vijana walijitahidi kutafuta goli ili angalau waweze kwenda mapumziko wakiwa na goli lakini juhudi zao hizo hazikufua lolote mbele ya walinzi walioonekana kuelewana katika kuzuia mipira kwenye safu yao ya ulinzi.
Haikuweza kuchukua muda katika kipindi cha pili pale Martial alipowaadhibu kwa mara nyingine Chelsea akimalizia mpira bora kabisa dakika ya 65 ya mchezo na kufanikiwa kuwa mbele kwa magoli mawili kitu kilichowavunja zaidi Chelsea kuona kama wangeweza kuwa na ahueni ya kusawazisha idadi hiyo ya magoli.
Hazikuzidi dakika hata mbili za mchezo ambapo Rashford aliandika bao jingine baada ya kupokea pasi nzuri sana kutoka kwa Pogba na kuwaacha walinzi wa Wanadarajani hao wakiangaliana tu. Karamu ya mabao iliweza kuhitimishwa na usajili mpya, James ambaye aliweza kuandika goli lake na kuweka historia mapema akitokea benchi.
Hadi sasa Chelsea wana wakati mgumu wa kuhakikisha wanapata matokea katika mechi zao ili kuweza kujinusuru maana kihistoria ni miaka mingi sana tabgu walipowahi kupoteza mechi zao kwa idadi kama ile ya magoli.


Issa
Lampard ni noma sana