Manchester City bado wameendelea kuonesha uwezo wao wa pekee wakiwa uwanjani baada ya kuandika historia nyingine ya kuwaadhibu watani zao wa jiji Manchester United katika mechi iliyokuwa ya muhimu kati ya wawili hao huku kila mmoja akicheza soka safi na lenye kuvutia jambo ambalo lilivutia zaidi.
City ndiyo walikuwa wahitaji zaidi wa alama kutokana na kuuhitaji ubingwa wa ligi hiyo kwa nguvu zote, jambo hilo kwa hakika lilifanya mechi kuonekana ya kuviziana sana katika kipindi chote cha kwanza. Sio hivyo tu, pia, kimbinu timu zote mbili zilionekana kutawala vizuri kutokana na kufahamiana vizuri.
Katika kipindi kizima cha kwanza timu zote zilijihami sana na kutompa yeyote nafasi ya kusogelea lango lake kwa namna yoyote ile. Na jambo hilo lilifanya mechi ionekane ngumu sana katika kipindi hicho. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika kila timu haikufanikiwa kabisa kuona lango la mpinzani wake.
Baada ya shika nikushike za kipindi cha pili nyota wa kikosi hicho ambaye mara nyingi amekuwa akibeba kikosi hicho kwenye hali za hatari, Sane aliweza kubadilishana na Fernandinho na kuweza kutengeneza mpira uliomkuta Bernado Silva na kufunga goli lake ambalo kwa hakika liliwaacha njia panda United.

Wakati wakiwa bado hawajatulia kwa mara nyingine, Sterling akiwa kwenye kasi ya pekee alitumia upenyo ulioachwa na mabeki na kumtengenezea mpira mzuri sana Sane ambaye hakuweza kuuacha na kufanikiwa kuupitisha nyavuni kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango mwenye historia zake, De Gea.
Kwa matokeo hayo, City anapanda juu ya jedwali la ligi hiyo akiwa na uwezekano mkubwa wa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kutokana na tofauti ya alama zilizopo kati yake na Liverpool ambao kwa hakika walikuwa wanategemea United wafanye lolote ili wao waweze kuibuka washindi wa ligi hiyo msimu huu.
Arsenal nao hoi!!!
Mbali na kichapo hicho cha United kutoka kwa City hata upande wa pili wa matajiri wa jiji la London, Arsenal mambo hayakuwa sawa baada ya kukubali kupokea kichapo cha 3-1 kutoka kwa Wolves. Kwa hakika Wolves wamekuwa na msimu mzuri sana kwa klabu zenye majina makubwa kwa kuzisumbua sana na hata kuondoka na matokeo pale inapobidi.
Hiyo ni dalili ya ukomavu kwa klabu hiyo; kutokana na hilo kunafanya ile nafasi ya kupambania kucheza klabu bingwa kuwa bado ngumu hasa pale inapokuja wawili hao, United na Arsenal kukabiliwa na mechi ngumu mbeleni ambapo United atakutana na Chelsea na Arsenal atakuwa na Leicester. Jambo hilo bado linaleta ugumu sana kwa wawili hao kukaa juu.


Povel
City noma sana