Kurudi kwa UEFA

Ni ndani ya wiki nyingine ya mzunguko wa pili ligi ya mabingwa barani Ulaya ambapo timu nane zitashuhudiwa zikiumana viwanjani huku kila moja ikitafuta nafasi ya kufuzu kuelekea hatua inayofuata. Timu hizo zinakutana huku kila moja ikiwa tayari na matokeo ya mapema yaliyopatikana katika mechi za awali.

Hizi ndizo huwa ni hatua ngumu zaidi katika michuano hiyo kutokana na kila timu kuwa imejiandaa na ipo tayari kupambana ili kuweka historia ya kuvuka hatua hiyo. Japo, mara nyingi klabu ambazo hupata nafasi ya kusonga mbele zaidi ni zile ambazo huwa tayari zimewahi kushiriki mara kadhaa ndani ya kombe hilo maana kwa kiwango kikubwa uzoefu huhitajika.

Katika mechi hizo Borussia Dortmund watawakaribisha katika jiji lao Tottenham Spurs ambao katika mechi ya awali aliweza kupoteza kwa mabao 3-0 kitu ambacho hakiwapi matumaini sana endapo wataweza kusonga mbele ndani ya michuano hiyo mikubwa. Maana kibarua walichonacho ni kikubwa sana cha kushambulia na kuwazuia kabisa Spurs wasipate nafasi ya kufunga; pamoja na kwamba soka ni mchezo wa maajabu lakini jambo hilo linaonekana kuwa gumu.

Dortmund amekuwa vizuri sana msimu huu, kitu kinachomfanya aendelee kuongoza ligi yao kwa sasa pamoja na kupoteza michezo yake ambayo angeweza kushinda. Hivyo, ili kumfunga Spurs leo anahitaji utulivu mkubwa sana maana Waingereza hao sio wa kubeza na wanarudi viwanjani wakiwa na nguvu waliyoipata baada ya kuwazuia Arsenal wasipate ushindi mbele yao.

Ndani ya vikosi vyote kuna walakini juu ya baadhi ya wachezaji tegemezi kuwepo ndani ya vikosi vyao ambapo Dortmund wao wanaweza kuzikosa nguzo zao kama hali haitaweza kubadilika: Christian Pulisic, Schmelzer na Piszczek huku upande wa pili kama hali zitaendelea hivyo watakuwa uwanjani bila Dele Alli, Hary Winks, na Erick Dier.

Mechi nyingine inayotegemewa kuwa na ushindani ni ile itakayokuwa kati ya Madrid na Ajax. Ndani ya mechi hiyo Madrid wanapewa nafasi ya kusonga mbele japo kwa sasa imekuwa sio timu ya kuaminika sana kwenye mechi kubwa na za muhimu kama hizi. Anaingia uwanjani akiwa na matokeo mazuri ya mechi ya awali ambayo akiwa ugenini aliweza kushinda 2-1.

Leo, akiwa mbele ya mashabiki wake na akiwa na maumivu ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Barcelona, ni imani kwamba kidonda hicho hakijapona bado; atarudi kupambana na Ajax ambao bado matumaini yao ya kusonga mbele yapo, wakiwa na goli moja mkononi kitu ambacho Madrid nao wana kibarua bado kuulinda ushindi wao.

Wanaingia uwanjani huku wakimkosa mlinzi wao wa wakati wote Sergio Ramos aliyepata kadi nyekundu na Marcos Llorente ambaye yupo majeruhi. Huku wapinzani wao watawakosa Carel Eiting na Lisandro Maggalan kama hali hazitabadilika. Kama Madrid atarudi na ari ya kupambana hii haiwezi kuwa mechi ngumu kwake kabisa kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu alioujenga ndani ya michuano hiyo.

Tuwatazame usiku wa saa 5!

Acha ujumbe