Furaha ya mchezaji katika maisha yake ya soka ni kuona kwamba anatengeneza wasifu wa pekee ambao huweza kuwa tofauti na mtu mwingine kitu ambacho humfanya yeye kuwa na upekee fulani hata anapoendelea kukua kisoka. Jambo hilo huchagizwa pia na kuchezea klabu zenye historia kubwa na ushawishi mkubwa kisoka.
Mbali na hayo kila mchezaji hutamani sana kucheza kwenye klabu ambayo kwake haiwezi kuwa na ukame wa vikombe kwa angalau misimu miwili au hata msimu mmoja. Kitu hicho mara kadhaa huwafanya wachezaji wapende kujiunga na klabu za aina hiyo ili waweze kutimiza ndoto zao za muda mrefu katika soka.
Wakati United ikianza kuimarika kwa sasa chini ya mwalimu Ole Gunner zimeanza kuzagaa taarifa kwamba mchezaji wa kimataifa kutoka Ufaransa anaonekana kuanza kutamani maisha ya Hispania kwa kuanza kuona kuna haja ya yeye kwenda kucheza soka lake katika taifa hilo kwa msimu ujao.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 kwa mara ya kwanza alianza kuhusishwa kujiunga na miamba wa Hispania wakati ambao Mourinho alikuwa anahudumu kikosini hapo baada ya kuwa anakosa namba ya kucheza mara kwa mara kutokana na migongano na mwalimu huyo. Lakini baadaye aliweka mambo sawa na amerejea kwenye jina lake halisi ambalo wengi wanalifahamu la kiwango kile alichokuwa nacho.

Pogba na wakala wake Mino Raiola wanaangalia njia ya kutoka kikosini hapo na kujiunga na miamba wa Hispania, Madrid hivi karibuni wakiamini kwamba ni jambo linalowezekana kutokana na sajili zinazotegemewa kufanywa na kikosi hicho cha wazee wa Los Blancos kutaka kujisuka upya.
Kwanini wamuwinde na ugumu uko wapi?
Madrid watamuangalia Pogba kama mbadala kwa Modric qmbaye umri wake kwa sasa umesogea akiwa na miaka 33 na anahitaji msaidizi ili kupata wakati wa kupumzika. Mshindi huyo wa tuzo ya Ballon d’Or amekuwa na misimu inayotafsirika vyema sana ndani ya ardhi hiyo kwa kutwaa vikombe vingi ndani ya ligi na michuano mingine mikubwa.
Jambo linaloonekana kuleta ugumu kumnasa mchezaji huyo ni suala la ada ya uhamisho kutoka kwake, hilo linatokana na kiwango ambacho United walitumia kumnasa nyota huyo kuwa ni cha juu mno. Kwa mwaka 2016 aliposajiliwa kutoka Juventus iligharimu £89m, kiwango hicho kimekua kutokana na uwezo, msaada na mataji aliyonayo mchezaji huyo.
Kama wakifanikiwa kumnasa si haba kwa Madrid kuanza kurejea kwenye ubora wao. Na kupitia wao tuanze kutegemea makubwa sana kutoka kwa mchezaji huyo na kuiona Madrid hiyo ikianza kurejea upya kwenye kinyang’anyiro chake cha ushindani mkubwa zaidi.


Mariam mtandama
Safi