Haya ni kama mafuriko yanayowakuta Madrid kila wanapojaribu kujinasua kwa kujishikilia katika majani yanayopatikana ndani ya mto waliomo. Inaweza kuwa sio dalili njema sana kwa timu ambayo ilikua mshindi wa kombe la Mabingwa Ulaya kutoka ndani ya michuano hiyo mapema kiasi hicho na kuwaachia wengine ushindani kuelekea hatua inayofuata.
Katika pacha yao Madrid alikuwa anaongoza kwa magoli 2-1 ambayo aliyapata ugenini kwenye mechi yake ya awali kabisa. Lakini kwa sasa wamekuwa sio wao tena kutokana na kuruhusu idadi kubwa sana ya magoli wakiwa nyumbani kwa mara nyingine mbele ya Ajax kwenye mechi ya marudiano.
Katika mechi iliyopigwa usiku wa jana walifungwa na Ajax magoli 4-1 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 3-5, kitu ambacho hana historia nacho kwa kiasi kikubwa ndani ya michuano mikubwa ya UEFA. Akiwa ametolewa mapema ataungana na wenzake waliokwishapokea vichapo na kutolewa mapema sana ndani ya mechi hizo.
Msimu huu wamekuwa hawaeleweki kabisa juu ya aina gani ya matokeo wanayapata na tatizo kubwa likiwa ni lipi kwa sababu kama mpira unachezwa lakini hawaoneshi kama kikosi chao kimekaa kiushindani kitu ambacho kiuhalisia kinawagharimu sana msimu huu na kushindwa kupata matokeo yanayoridhisha.
Kwa aina hiyo ya matokeo wengi lazima wataendelea kukumbuka uwepo wa Ronaldo kikosini hapo kwa sababu alikuwa ni zaidi ya mchezaji kutokana na falsafa yake ya kuhamasisha timu kupigania matokeo mazuri na moyo wa upambanaji uliomfanya kuwa nafasi ya juu kabisa katika historia ya soka.
Kuna wakati masuala ya kimfumo ndani ya kikosi hicho yanaweza kuwa na changamoto kubwa kuifanya timu hiyo iweze kupata ushindi. Maana hata ikisingiziwa kwamba kikosi hicho kimechoka kutokana na kupata mafanikio mengi lakini pia ni wachezaji walewale ambao walichukua ubingwa na kikosi hicho; hivyo hata suala la kimfumo bado ni tatizo kubwa.
Kwa mwenendo huo Solari ni vigumu sana kwake kukabidhiwa kikosi cha timu hiyo ili akinoe kutokana na matokeo ya mwanzo kabisa ya kushindwa kukimudu na kuwafanya kupoteza mechi tatu mfululizo katika ardhi yao wenyewe na mbele ya mashabiki wao ambao siku zote hawajawahi kuwaangusha.
Mbali na dozi hiyo ya Madrid, pia upande wa pili Dortmund alikubali kufungwa na Spurs akiwa nyumbani mbele ya mashabiki zake. Ikumbukwe katika mechi ya awali pia aliweza kupigwa goli 3-0 mbele ya mashabiki wa Spurs ambao wanaipa nguvu ya kupambana timu yao. Kutokana na hilo sasa wataungana na mwenzake Madrid kuendelea kushuhudia wenzao wakisonga mbele kwenye michuano hiyo yenye heshima kubwa.


Hopemwaikuka
Nc