Klabu ya Manchester City imefanikiwa kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya Uingereza baada ya kufanikiwa kupata ushindi wa mabao manne kwa mawili dhidi ya klabu ya Crystal Palace.
Manchester City ambao walikua wakishika nafasi ya tatu kabla ya mchezo wa leo wanafanikiwa kukwea mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Palace mchana wa leo wakiwa ugenini katika dimba la Selhurst Park.Mchezo huo uliopigwa pale Selhurst Park mchana huu ni wenyeji waliofanikiwa kupata bao la uongozi kupitia kwa mshambuliaji wao Jean Mateta dakika ya 3 ya mchezo kabla ya Kevin de Bruyne kusawazisha dakika ya 13 ya mchezo na kufanya mchezo kwenda mapumziko kwa sare ya bao moja kwa moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Man City wakionekana kua na moto kwelikweli wakihitaji kupata goli la pili, Juhudi zao zilizaa matunda kwani mnamo dakika ya 47 tu walifanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa kijana mdogo Rico Lewis.
Vijana wa kocha Pep Guardiola hawakuonekana kuridhika kwa mabao mawili kwani dakika ya 66 Earling Haaland alifanikiwa kufunga bao la tatu kabla ya Kevin de Bruyne kupiga msumari wa mwisho, Huku bao la pili la Palace likifungwa na Odsonne Odouard dakika ya 86 ya mchezo.Mchezo ulimalizika kwa Manchester City kushinda mchezo na kufanikiwa kuwafikia vinara Liverpool kwa alama ambapo mpaka sasa wana alama 70 kwa pamoja, Lakini Liverpool bado wanaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Arsenal wao wakiwa nafasi ya tatu na alama zao 68.