Mchezaji wa Barcelona Hector Bellerin anaamini kuwa kocha wa timu hiyo anahitaji muda wa kujenga timu huku beki huyo akitarajia kuwa sehemu ya ujenzi wa timu hiyo ya mafanikio hapo Camp Nou.

Barcelona walionyesha nia yao katika soko la usajili kabla ya msimu mzima wa kwanza wa Xavi kama kocha mkuu, huku Robert Lewandowski, Raphinha na Jules Kounde wakiwa miongoni mwa wachezaji wengi waliosajiliwa kuwasili Camp Nou.
Bellerin alikuwa ni miongoni mwa waliosajiliwa, akiwasili katika klabu hiyo ambapo alianza kazi yake kwa mkataba wa mwaka mmoja. Barca ilishindwa kufuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini wapo pointi 1 nyuma ya vinara wa Laliga Real Madrid, baada ya kushinda mara 10 katika mechi 12.
Na beki huyo akapendekeza kuwa Xavi, amabye alichukua nafasi ya Ronald Koeman aliyetimuliwa Novemba mwaka jana, huenda akahitaji muda zaidi sawa na ambao walipewa makocha wa Manchester City Guardiola, na Liverpool Jurgen Klopp.

Beki huyo hakusita kusema kuwa “Kandanda sio nyeusi wala nyeupe, Kuna sababu nyingi ambazo zinaweza kuathiri. Kuna wachezaji wengi waliosajiliwa huku miradi hii inachukua muda kuzaa matunda, Klopp na Guardiola hawakushinda chochote katika msimu wao wa kwanza. Mambo huchukua muda”.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alisema kuwa ana furaha sana kuwa hapo na ni ndoto ambayo amekuwa nayo siku zote. Bellerin ambaye ni mchezaji wa zamani wa Arsenal angefurahia kubaki na Barca hadi mwisho wa msimu huu na kwasasa ana mkataba mmoja. Anapenda pia angeongeza mkataba lakini itategemea pande zote mbili.


