Mnamo mwaka 2002, Januari 23 FC Porto walimsajili Jose Mourinho kuwa kocha wao mkuu, ni wakati huo Porto alikuwa wa tano kwenye msimamo wa ligi. Mourinho alifanya yake na kuweza kuipandisha nafasi mbili juu yaani kutoka ya tano hadi ya tatu, na cha zaidi akawaambia mwakani atakuwa bingwa wakamuamini na kumpa muda.
Msimu wa 2002/03, Mourinho aliandaa timu akiwa na wachezaji tegemezi kama Deco, Carvalho, Postiga na baadaye Maniche, kweli mambo yalikuwa mambo akawa bingwa wa Ureno pia, akachukua Tace de Portugal na UEFA Cup. Hakuishia hapo kwani 2004 akachukua ligi ya Ureno na lile la klabu bingwa barani Ulaya, asikuambie mtu hapa wasifu wa Mourinho ulipanda sana. Hivi unafikiri timu gani isingemuhitaji Mourinho, aaaah wapi, hatimaye Chelsea wakanasa saini yake.
Mambo yakaenda vizuri miaka miwili mfululizo, hatimaye kupanda na kushuka mara kafukuzwa Chelsea mara kaenda Madrid mara Inter hatimaye akarudi tena Chelsea. Walau alianza vizuri na kunyakua taji la ligi msimu wa 2014/15 ila 2016 alitupiwa virago baada ya kutaka kuishusha daraja timu, Chelsea ilikuwa mdebwedo dhaifu, vibonde wa kutupwa au tuseme timu ilikuwa dhohofu hali.
Bwana eeeh, hatimaye akaja Man United alijitahidi walau kuwapa Europa ligi na Carabao Cup ila walikuwa nafasi ya saba kila uchwao, yaaaah, mashabiki pinzani waliimba sana kuwa timu imehamia mtaa wa saba kutwa kuinanga Man United. Man united wakaona isiwe taabuMourinho akatemwa 2019 mwanzoni kabisa.
Wahenga husema mpewa hapokonyeki yaani aliyepewa hata ufanyaje huwezi kumpokonya, basi Mourinho akalamba shavu Tottenham baada ya Pochettino kutimuliwa. Mourinho akaanza kazi kama kocha mkuu wa Tottenham, akashinda mechi mbili za kwanza zote akishinda kwa mabao 3-2 watu wakaona yes walau tunapumua.
Ila gundu likaanza, akafungwa mechi 2 mfululizo. Mhhhh, ni kweli aliikuta timu ikiwa ya 14 akaileta hadi ya 7 ila ikumbukwe kuwa katika kipindi hicho mtu wa 5 na wa 14 walitofautiana alama 3 tu. Mpaka leo ameshindwa kuziba hilo pengo la alama 3 amejitahidi kuipunguza moja tu, haaahaahaa, yah, inabidi tucheke katika mechi 16 alizocheza ameshindwa kuzipata alama alizozihitaji ili kufika walau nafasi ya tano!
Uzuri Mourinho hakuahidi kuwa atawapa kombe la ligi ya Uingereza ila aliahidi atawapa FA Emirates Cup. Ajabu ni kuwa juzi tu aliiona joto ya jiwe baada ya kukubali kichapo tena kwa mikwaju ya penati kutoka kwa Norwich City tuseme tu aliyaaga mashindano hayo.
Swali la kujiuliza, Mourinho anakwama wapi majeruhi au, duuuuh ni kweli Kane, Son, Lloris na Sissoko wote ni majeruhi na wote hao ni tegemeo, au kushuka kwa viwango? Ndiyo, Moura na Wanyama kweli wameshuka, swali je, nini kilisababisha amuuze Eriksen wakati tayari ana majeruhi wa kutosha?
Ukweli amesajili jembe, Steven Bergwijn linaloonesha kazi kubwa ila tunamtaka Mourinho yule aliyemleta Michael Essien, Drogba na Carvalho pale Darajani. Ukweli tunataka Mourinho asuke kikosi kama kile cha Porto 2002 au kile cha Chelsea 2004 yaani asuke timu ya ushindani siyo vinginevyo.
Tunataka aifanye Tottenham iwe kama ile Chelsea ya 2004, ile iliyomtingisha Sir Alex Ferguson ndani ya miaka miwili mfululizo asijue la kufanya. Ile iliyofanya umma ukubali kuwa Mourinho ni Special One.
Uzuri Pochettino ameweka rekodi ya kufika fainali ligi ya mabingwa Ulaya. Kazi ipo kwa Mourinho maana kufika UEFA robo fainali sidhani maana kumfunga Leipzig kwake ni kibarua kizito kidogo ingawa inawezekana ila zinahitajika dua za kutosha.
Japo walau hata wamalize nafasi za nne za juu ila kwa majeruhi wale loooooh sijui ila dua zinahitajika.yooooote tupa kule Mourinho ni Special One na anajua nini anafanya, ndiyo ila muhimu zaidi atuoneshe tu walau japo hata tushiriki Klabu Bingwa Ulaya mwakani kwenye suala la kuchukua Champions ligi nafikiri tutakuwa tunamuonea. Tusubiri tuone maana mwezi wa tano siyo mbali.


Ester
Mourinho apumzike kwanza ili ajiweke vizuri
Povel
Gud news
Ester jackson
Mourinho kashazeeka apumzike tu