Kuna baadhi ya mameneja hawajawahi kubahatika hata mara moja kunyanyua ndoo ya klabu bingwa Ulaya pamoja na historia nzuri waliyonayo katika soka hilo. Kama ilivyo historia ya michuano hiyo kwa kocha anayefanikiwa kuchukua taji hilo huweza kujijengea historia safi yenye tija katika maisha yake kisoka na katika utwaaji wa tuzo na mataji mengine.
Antonio Conte
Pamoja na kuwa na historia pana ndani ya Uingereza akiwa na Chelsea na Italy pia, lakini kocha huyo hana bahati kabisa ya kunyanyua ndoo hiyo ambayo wengi huamini ni kipimo tosha cha kujua uiamara na ubora wa kocha katika kupangilia kikosi alicho nacho. Alishindwa kufanya vizuri alipokuwa na Juve ambapo alifanikiwa kufika nafasi ya robo fainali ya michuano hiyo.
Unai Emery
Ameweza kuongoza klabu zenye heshima na majina makubwa lakini hajawahi kufanikiwa kunyanyua kombe hilo akiwa na klabu hizo pamoja na kuwa na majina makubwa ndani ya kikosi chake. Alianza safari yake akiwa na Sparta Moscow, akaja kuiongoza Valencia, baadaye akajiunga na Valencia akaja upande wa pili wa Sevilla na msimu uliopita kabla ya kusaini na Arsenal alikuwa na PSG ambapo alishindwa pia kutwaa kikombe hicho.
Didier Deschamps
Wengi wanasema hata kombe la dunia ameweza kushinda kutokana na kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa. Jambo hilo linaonesha kwamba sio suala la kimbinu lililomfanya Mfaransa huyo kutwaa kombe hilo la dunia 2018. Pamoja na hayo, hajafanikiwa kabisa kushinda UEFA tangu alipokuwa na Monaco na baadaye kuiongoza Marseille, hivyo bado ana deni ili kukamimilisha wasifu wake.
Mircea Lucescu
Kocha huyo pamoja na kuwa na historia tangu akiwa mchezaji hadi nafasi ya pekee kuweza kuwa mwalimu hajafanikiwa kabisa kushinda taji hilo. Akiwa amefundisha klabu nyingi zenye majina na kuweza kuzijenga katika ushindani lakini imekuwa vigumu kwake kutwaa taji hilo. Baadhi ya klabu zilizopata huduma yake ni Galatasaray, Shakter Donetsk, Inter Milan, Besktas na Rapid Bucharest.
Otto Rehhagel
Amehudumu na Werder Bremen kwa kipindi cha miaka 14 na kufanikiwa kunyanyua makombe mengi makubwa na klabu hiyo ndani ya jiji hilo yakiwemo DFB-Pokals, German Supercup na mafanikio mengine mengi. Lakini hajaweza kabisa kufanikiwa kuchukua kombe hilo lenye historia pamoja na kukaa kwa muda mrefu na klabu hiyo; pia klabu nyingine alizohudumu ni Kaiserslautern.

