BAADA ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Simba, Kocha Mkuu wa kikosi cha Dodoma Jiji, Masoud Djuma amefunguka kuwa sababu ya kupoteza mchezo huo ni kutokana na uchovu wa safari.

Simba iliibuka na ushindi huo jana jumapili kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar ambapo mabao ya mchezo huo yalifungwa na Moses Phiri, Habibu Kyombo huku Abdallah Shaibu ‘Ninja’ akijifunga.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Djuma alisema: “Kwanza tunamshukuru Mungu kwa mchezo kumalizika salama na hakuna mchezaji yeyote aliyepata majeraha.

“Sababu ambayo imetufanya tufungwe ni wachezaji wangu walikosa umakini kwenye eneo la mwisho na nadhani ni kutokana na ukubwa wa timu ambayo wanacheza nayo.

“Walikuwa wakifika kwenye eneo la mwisho wanakosa umakini hivyo wanashindwa kumalizia zile nafasi ambazo wanazipata.

“Kitu kingine ni kutokana na uchovu wa safari hilo pia limechangia kwani tulicheza mechi hivi karibuni na usiku huo huo tuliondoka kuja Dar hivyo wachezaji walichoka sana ndicho kilichochangia matokeo haya ya leo.”

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa