ZIKIWA zimesalia siku nne tu, kabla ya kufanyika kwa tukio lao kubwa la
siku ya Simba, uongozi wa Simba umeweka wazi kuwa umeandaa Sapraizi
kubwa ya utambulisho wa mastaa wapya wa timu hiyo katika kilele cha siku
ya Simba ‘Simba day’ itakayofanyika siku ya Jumatatu.
Simba wanatarajia kufanya sherehe za tamasha lao la siku ya Simba Agosti
8, mwaka huu ambapo tamasha hilo litafanyika kwa mara ya 14 mwaka huu
mara baada ya kuasisiwa mwaka 2009.
Tamasha hilo hutumika kama sehemu ya kutangaza kikosi kipya cha Simba
kwa msimu husika, ambapo pamoja na burudani mbalimbali hucheza mchezo wa
kirafiki ambapo taarifa za ndani zinaeleza kuwa wanatarajia kucheza
dhidi ya timu ya St. George ya Ethiopia.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kilisema: “Tunatarajia kuwa
na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu ya ST. George ya
Ethiopia ambao tumewaalika kwa ajili ya mchezo wa kilele cha siku ya
Simba na tunawatarajia watatua nchini muda wowote kutoka sasa.”
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema: “Mashabiki wa Simba
wakae tayari kwa ajili ya tamasha letu kubwa, kuelekea tamasha hilo tuna
sapraiz kubwa ya utambulisho wa wachezaji wapya kwani bado hatujamaliza
usajili.
“Tutaitikisa nchi kwa utambulisho wa wachezaji hawa na burudani kubwa
ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya wageni ambao tumewaalika.”