AFISA Habari wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally ameamua kuvunja ukimya baada ya maneno mengi kuzungmzwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu sakata la kujiuzulu kwa CEO Barbara ikihusishwa kuwa ndani ya klabu hiyo kuna mpasuko mkubwa na mgogoro uliomfanya CEO kung’atuka.
Ahmed kupitia mtandao wa Instagram yake aliandika ujumbe ukiwataka wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba SC kusimama imara kwa pamoja ili kutimiza malengo ya klabu huku akisisitiza kuwa ‘Wanataka Tupoteane ili washinde Vita Kiurahisi’ hii ni kwa wapinzani wao.
“Mengi yamezungumzwa wiki hii, Muhimu sisi tunasonga mbele tukiangalia yaliyo muhimu kwetu ambayo ni kucheza mpira.
“Wadada wetu wa Simba Queens wanaelekea Arusha kwenye mchezo wa ligi kuu ya Wanawake dhidi ya Tigers Fc.
“Wakati huo huo Simba Senior team inaendelea na maandalizi kuelekea mechi yetu ya December 18 dhidi ya Geita Gold FC.
“Miluzi mingi humpoteza mbwa lakini sisi miluzi mingi inatuongezea umakini.
“Wanataka tupoteana ili washinde vita kiurahisi nasi tunawaambia tutaendelea kusimama imara na pamoja mpaka malengo yetu yatimie. Tuishi humo wana Simba” Alimaliza kwa kusema hivyo Ahmed Ally.
Siku ya Jumamosi jioni 10/12/2022 Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Barbara Gonzalez alithibitisha kwenye akaunti yake kuwa ameandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo mwezi Januari mwakani, ili kuendelea na mambo yake mengine lakini pia kutoa fursa kwa wengine.