TAARIFA za uhakika ambazo nimezipata ni Uongozi wa Azam FC, umetuma ofa kwa kocha mkuu wa KMC FC, Abdulhamid Moalin arejee kwa mara nyingine ndani ya viunga vya Azam Complex.
Azam FC ilishatuma ofa ya kwanza kwa Kocha Abdulhamid Moalin ambayo ameikataa baada ya kuwa na maslahi ambayo bila shaka Kocha Moalin ameona hakuna sababu ya kuiacha KMC FC ambayo inashika nafasi ya tatu kwenye ligi.Baada ya Ofa ya Kwanza kukataliwa Azam FC imetuma ofa ya pili kwa Abdulhamid Moalin, Ofa ambayo bado hajaijibu mpaka sasa.
Inadaiwa Abdulhamid Moalin maamuzi ya kuondoka au kubaki KMC FC anayo mwenyewe japo ofa ya sasa ni kubwa mno.
Chanzo cha taarifa hii kilisema kuwa: “KMC FC kwa ofa waliyotuma Azam FC hawana uwezo wa kumpa, hivyo kama Moalin ataamua kuondoka basi hakuna kipingamizi tena.”Alipotafutwa msemaji wa Azam FC Hasheem Ibwe ili kujua uwepo wa taarifa hizi alisema kwa wakati huu wanautazama kwanza mchezo wao na Mashujaa FC ambao utachezwa jana Lake Tanganyika, Kigoma.
Viongozi wa KMC FC mpaka sasa bado hawaelewi wafanye nini maana Moalin kwa kipindi kifupi ndani ya KMC FC ametengeneza kikosi bora na cha ushindani. Chanzo kilipigilia msumari.