Bado bundi analia mitaa ya Msimbazi kwani mambo yamekua hayaelewiki kila uchwao kwa klabu ya Simba ambapo leo wamedondosha alama tena katika mchezo wa ligi kuu ya NBC mbele ya klabu ya Ihefu.
Simba wamelazimishwa sare na klabu ya Ihefu Fc katika mchezo uliopigwa mkoani Singida katika dimba la Liti, Jambo ambalo linaendelea kuididimiza klabu hiyo kwani walipaswa kushinda mchezo huo ili kupunguza pengo la alama baina yao na watani zao klabu ya Yanga.Mchezo huo ulionekana kua wa pande zote kwani Ihefu nao walionekana kuhitaji matokeo ya ushindi na ndio waliofanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao Duke Abuya na mchezo kwenda mapumziko kwa Ihefu kuongoza kwa bao moja kwa bila.
Kipindi cha pili kilianza Mnyama akionekana kua na usongo wa kupata matokeo na kupeleka mashambulizi mara kwa mara langoni mwa Ihefu, Mpaka pale dakika ya 72 ya mchezo wanafanikiwa kupata mkwaju wa penati uliowekwa kambani na Clatous Chama na kufanikiwa kusawazisha goli na ubao kusoma moja moja.Mabingwa hao wa zamani wa ligi kuu walionekana kulisakama lango la Ihefu angalau waweze kuvuna alama tatu muhimu, Lakini haiwezekana kwani mchezo ulimalizika kwa sare ya bao moja kwa moja na ni wazi sasa Simba anaendelea kua nyuma kwa alama 6 wakiwa wamecheza michezo sawa mpaka sasa.